0
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaendelea na
maandalizi ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa
kuboresha daftari la wapiga kura ili kuweka taarifa
za walengwa wakiwemo watakaopiga kura baada
ya kufikisha umri wa kupiga kura.
Aidha, itawahusu walioshindwa kupiga kura katika
chaguzi zilizopita kutokana na sababu
mbalimbali. Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na
Ofisa Uchaguzi wa Tume hiyo, Adam Nyando
wakati akikabidhi taarifa za Uchaguzi Mkuu wa
2015 kwa mkoa wa Pwani.
Alisema, baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa
mwaka 2015, wameanza maandalizi ya uchaguzi
mkuu ujao na si kwamba kwa sasa Tume imelala.
“Watu wanafikiri uchaguzi ukishaisha ndio kazi
imekwisha kumalizika kwa uchaguzi mmoja ni
maandalizi ya uchaguzi ujao kwani kwa sasa
tunaendelea na uboreshaji wa daftari la
wapigakura pamoja na kura za maoni,” alisema
Nyando.
Alisema uchaguzi uliopita ulikwenda vizuri na
hakukuwa na matatizo makubwa licha ya
matumizi ya mfumo mpya wa BVR, lakini matokeo
yake umekuwa mfumo mzuri na umepata
mafanikio makubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo,
akizungumza alitumia fursa hiyo kuwapongeza
Watanzania kwa kufanya uchaguzi mzuri
usiokuwa na vurugu wala uvunjifu wa amani.
Ndikilo alisema nchi nyingine kipindi cha
uchaguzi ni kipindi kibaya cha uvunjifu wa amani,
ikiwa ni pamoja na umwagikaji mkubwa wa damu,
hasa kwa pande zisizokubaliana matokeo.
“Uchaguzi ulienda vizuri licha ya changamoto
zilizojitokeza za hapa na pale lakini watu
walivumiliana na kukubaliana na matokeo
kilichobaki sasa ni kufanya kazi ili kuwaletea
maendeleo wananchi, kikubwa ni tume kufanyia
kazi changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na
usafiri na ucheleweshwaji wa matokeo kwa baadhi
ya sehemu,” alisema Ndikilo.
Akikabidhi taarifa hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Ofisa Uchaguzi wa mkoa, Shangwe
Twamala alisema mkoa huo umepata nakala 47
ambazo zitasambazwa kwa wadau mbalimbali wa
uchaguzi.
Alisema taarifa hizo zitasambazwa kwenye ofisi
za mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi
wa halmashauri za miji na wilaya na taasisi za
elimu ya juu.

Chapisha Maoni

 
Top