0

ALIYEKUWA mgombea urais kupitia mwamvuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward
Lowassa amewataka vijana wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumlinda
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe
kama nyuki wanavyomlinda malkia wao.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, alitoa kauli hiyo wakati akifungua
kikao cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana
(Bavicha) jijini Dar es Salaam jana.
Waziri mkuu huyo wa zamani, pamoja na mambo
mengine aliwataka vijana wa chama hicho kuacha
vita vya ndani kwa ndani na badala yake
washikamane na kuwang’ang’ania viongozi
wanaowaongoza.
“Tuache vita vya ndani kwa ndani, Mbowe ndiye
mwenyekiti wetu wa chama…tumlinde kama nyuki
wanavyomlinda malkia wao. Mtu akishakuwa
kiongozi tumg’ang’anie,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye alijiunga na upinzani mwishoni
mwa mwaka jana alisema kumekuwapo na
kawaida ya kuibuka kwa makundi uchaguzi
unapomalizika.
Azungumzia uchumi
Katika mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia
uchumi ambapo alisema hivi sasa maisha ya
Watanzania walio wengi hayana uhakika, huku
matumaini kidogo yakielekezwa kwa watu
wachache.
“Binadamu anaishi kwa matumaini, lakini mambo
yanayoendelea hapa nchini hayatoi matumaini
hayo…hali ya uchumi inakwenda vibaya sana,
kuna rafiki yangu mmoja ana msamiati wake
anasema maisha ni pasua kichwa hivi sasa kwa
sababu hayana uhakika,” alisema Lowassa.
Aidha Lowassa alieleza kusikitishwa kwake kwa
baadhi ya watu kuacha kuzikana kwa sababu ya
siasa ambapo alisema hayo ni mambo ya ovyo.
Ajivunia vijana
Katika hotuba yake hiyo, Lowassa aliwapongeza
Bavicha kwa kutii maelekezo ya Mbowe kuhusu
kusitisha uamuzi wao wa kwenda Dodoma kuzuia
Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Niwapongeze kwa kutii maelekezo ya mwenyekiti
wetu, najua haikuwa rahisi, mlikuwa
mmeshajipanga lakini maelekezo ya mwenyekiti
ni mazuri, vitu vingine si lazima uende mbali
sana ni kama kwenye simu kwamba ‘message
sent’ mlifikisha ujumbe mahsusi hata kama
hawakubaliani lakini ujumbe umefika.
“Wala msione aibu mnachofanya, vijana
mngefanya tofauti ningeshangaa, nyie ndio
chachu ya mabadiliko lazima mje na kitu kipya na
mawazo mapya, ninyi ni jeshi la chama.
“Kwa uzoefu wangu CCM lazima watakwenda
kumtambulisha mwenyekiti wao mpya katika
Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, hivyo
wananchi wenyewe wataangalia na kupima kama
Chadema wanazuiwa kwa nini wapinzani wazuiwe,
waachane wapate tabu kujieleza kwa umma”
alisema Lowassa huku akishangiliwa.
Kuhusu uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli
hivi karibuni, Lowassa aliuponda na kusema ni wa
kibaguzi kwa sababu umewatenga vijana wa
vyama vya upinzani.
“Kama wewe ni CCM utakuwa mkuu wa wilaya,
mkoa na hata mkurugenzi wa halmashauri lakini
hali ni tofauti kwa vijana wa upinzani,
wanabaguliwa utadhani si Watanzania.
“Hili ni jambo la kutafakari na kukemea kwa sabu
ajira ni tatizo hapa nchini, lakini hata hizo chache
zinatoka kwa kubaguana pamoja na jitihada zote
lakini hazisaidii,” alisema.



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top