Chama cha NCCR – Mageuzi kimemvua
uanachama makamu mwenyekiti wake (Bara),
Leticia Ghati (pichani) kikimtuhumu kujihusisha
na migogoro ndani ya chama na tuhuma nyingine
za kijinai.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia
aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa uamuzi
huo umepitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya
chama hicho.
Mbunge huyo wa Vunjo na mwenyekiti mwenza
wa Ukawa, alisema makosa mengine aliyokutwa
nayo Ghati ni pamoja na kukashifu na kutoa
tuhuma dhidi ya kiongozi wa chama nje ya
utaratibu na kuhujumu chama wakati wa
uchaguzi.
“Kwa makosa hayo ambayo Leticia Ghati
aliyatenda wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015
Halmashauri Kuu ya Taifa, inamsimamisha
uongozi na kumvua uanachama,” alisema
Mbatia.
Mustakabali wa chama
Akizungumzia mustakabali wa chama hicho katika
Ukawa, Mbatia alisema Halmashauri Kuu ya
chama hicho itaendelea kusimama imara
kuhakikisha umoja huo unakuwa bora na taifa
linapata Katiba kama yalivyokuwa malengo ya
kuanzishwa kwake.
“NCCR tutahakikisha Ukawa unaboreka na
kusimama imara kwa ajili ya kupata Katiba,
tumeazimia kuunga mkono jitihada za
kuunganisha vyama vinavyounda umoja huu ili
kufikia lengo la kuwa na chama kimoja cha siasa
chenye nguvu,” alisema Mbatia.
Mbatia pia alizungumzia hali ya kisiasa na
kidemokrasia nchini na kusema chama chake
kimebaini kuwa taifa linaongozwa kwa matamko
ya Rais John Magufuli badala ya kufuata Katiba,
sheria na kanuni.
Alisema demokrasia imeendelea kukiukwa huku
uhuru wa kujieleza ukiendelea kudidimizwa na
akatolea mfano mwenendo wa Bunge ambao
alisema licha ya kuwa chombo cha kikatiba
chenye mamlaka kamili ya kujiendesha, limeanza
kuingiliwa katika uendeshaji wake kwa wabunge
kunyimwa fursa ya kujadili kwa uwazi masuala ya
Watanzania.
Alisema NCCR inakemea matu- mizi ya nguvu za
dola kupitia Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya
hadhara ya vyama vya siasa, kuwakamata na
kuwaweka rumande viongozi wa kisiasa na
kuwashtaki kwa makosa mbalimbali.
“NCCR Mageuzi tunalaani tabia ya polisi
kuwakamata na kuwahoji mara kwa mara
viongozi wa kisiasa na kuwashtaki kwa makosa
mbalimbali… vitendo hivi ni ukiukaji wa uhuru na
haki za vyama vya siasa katika kufanya kazi zao,”
alisema Mbatia.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni