0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi
wa mkoa wa Dodoma pamoja na Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la
bandari kavu ili mkoa huo uweze kupokea na
kuhifadhi mizigo na kurahisisha biashara kwa
mikoa jirani.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Julai 20,
2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi
wa mkoa wa Dodoma mara baada ya kuweka jiwe
la msingi kuashiria uzinduzi wa awamu ya
kwanza ya ukarabati na upanuzi wa uwanja wa
ndege wa Dodoma.
“Ninazo taarifa kuwa Benki ya Dunia kupitia
shirika la Local Investment Climate (LIC) tayari
wametenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100
kwa ajili ya kujenga bandari kavu na tayari fedha
hizo zimeshapokelewa na Mkoa wa Dodoma kwa
ajili ya kazi hiyo.”
“Uzuri wa mkoa wa Dodoma kuna reli. Kwa hiyo
makontena yanayoenda Burundi na mahali
kwingine yatashushwa hapa na kukaa kwenye
bandari kavu; hivyo, wafanyabiashara watachukua
mizigo yao hapa badala ya kupata shida ya
kuyafuata Dar es Salaam kama ilivyo sasa,”
amesema.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano itoe wataalam ili washirikiane na
CDA kufanikisha kazi hiyo. Amesema hatua hiyo
itasaidia kurahisisha wananchi na
wafanyabiashara kupata huduma hiyo kwa urahisi
na umbali mfupi tofauti na hali ilivyo sasa.
Ameuagiza pia uongozi wa CDA utenge eneo
maalum la kituo cha biashara (commercial hub))
ili Kanda zote zinazozunguka mkoa wa Dodoma
na nchi jirani wapate bidhaa mbalimbali kutokea
Dodoma.
“Kutokana na upanuzi huu na fursa
zinazojitokeza, hii iende sambamba na
kuwatengea maeneo maalum wajasiriamali badala
ya kuwaacha kuzagaa kila mahali,” amesisitiza
Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu upanuzi wa uwanja huo,
Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi huo
kutaziwezesha ndege zenye uwezo wa kubeba
abiria 90 zianze kutua kwenye kiwanja hicho na
kukuza fursa za kibiashara zinazohitaji usafiri wa
haraka na salama.
“Katika Ilani ya CCM, suala la ujenzi na uboreshaji
wa miundombinu ya viwanja vya ndege limepewa
umuhimu mkubwa sana na ndiyo maana leo
tunashuhudia utekelezaji wa ahadi za
Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha
upatikanaji wa fedha za ukarabati na fidia kwa
wananchi wa kata za Makole na Uwanja wa Ndege
ambao maeneo yao yametwaliwa na Serikali ili
kufanikisha upanuzi huu,” amesema.
Amesema uzinduzi huo ni mwanzo tu wa
utekelezaji wa miradi mingine ya kuboresha na
kupanua viwanja vya ndege nchini ambapo
Serikali kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ya
ndani na ya nje, itaendelea kuboresha zaidi
miundombinu na huduma nyingine za viwanja
vya ndege kama vile Mtwara na Mwanza
ambavyo amesema vitapanuliwa kufikia hadhi ya
kimataifa.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni viwanja vya
ndege vya Kigoma na Tabora ambavyo
vinaendelea kupanuliwa kwa kujenga majengo ya
abiria na maegesho ya ndege ili kufikia viwango
vya huduma za kimkoa; viwanja vya Shinyanga
na Sumbawanga vitapanuliwa kwa kuboreshwa
miundombinu na majengo yake kufikia hadhi ya
viwanja vya kimkoa; huku kiwanja cha ndege cha
Lindi kikiboreshwa miundombinu yake kufikia
hadhi ya kimkoa na kuweza kuhudumia viwanda
vinavyotokana na uchumi wa mafuta na gesi.
Amesema Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi
wa jengo la tatu la abiria (Terminal 3) katika
kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA) ambalo likishakamilika Desemba
2017 litahudumia abiria wapatao milioni 6 kwa
mwaka; ilhali kiwanja cha ndege cha kimataifa
cha Kilimanjaro (KIA) kinapanuliwa miundombinu
yake na jengo la abiria ili kiweze kuhudumia
abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia hadhara
hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Prof. Makame Mbarawa ameiomba Serikali
iendelee kuwekeza katika ujenzi wa uwanja wa
ndege wa Msalato ili ndege za kimataifa ziweze
kutua kwenye mkoa huo.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho amesema
Serikali imetoa sh. bilioni 11.8 kwa ajili ya kazi
hiyo na kwamba hadi sasa wamekamilisha
asilimia 60 ya ujenzi kwa kuweka lami umbali wa
km.2.0 kati ya km.2.5 zinazohitaji kukamilishwa
chini ya mradi huo.
Amesema hivi sasa ndege zinazoweza kuruka na
kutua kwa umbali huo zinaweza kuanza kutoa
huduma kwenye uwanja huo wakati wakiendelea
kukamilisha ujenzi wa mita 500 zilizobakia.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
TAA, Eng. George Sambali alisema ukarabati huo
ulianza Juni 24, 2016 na imechukua siku 27 hadi
sasa, kazi ambayo alisema inawezesha kiwanja
kutumika kwa ndege zenye uwezo wa kubeba
abiria hadi 90 na zenye mwendo wa kasi. Hata
hivyo, alisema kazi iliyobakia inatarajiwa
kukamilika baada ya miezi miwili.



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top