Ni nani aliyechochea mapigano ya karibuni huko
Sudan Kusini yalioanza Ijumaa, Julai 8,
yaliyosababisha zaidi ya watu 300 kuuawa na
nchi hiyo changa mwanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki?
Hilo ni swali linaloulizwa na watu wa nchi hiyo na
pia na jamii ya kimataifa. Aprili mwaka huu Rais
wa nchi hiyo, Salva kiir na makamu wake, Riek
Machar, waliunda Serikali ya mpito baada ya
kufikia mapatano ya amani mwaka mmoja
uliopita.
Mapatano hayo yalisitisha vita vya kienyeji
vilivyochomoza miaka mitano baada ya Sudan
Kusini kujitenga kutoka Sudan.
Kwa nini Kiir na Machar wanagombana tena mara
hii? Jibu ni kwamba Kiir anataka kubakia kuwa
rais wa nchi, lakini Machar ana tamaa.
Kiir na Machar wanawakilisha makabila mawili
makubwa katika Sudan Kusini, Wadinka na
Wanuer, ambayo yamekuwa yakihasimiana kwa
muda mrefu.
Mapigano yaliyoanza Desemba 2013. Mapigano
ya karibuni ni kwamba mara kadhaa lilichomoza
jina la mtu watatu: Paul Malong, Mkuu wa Majeshi
ya Sudan Kusini ambaye ni mtu mwenye siasa
kali za ukabila wa Kidinka na anapigania kabila
lipate nafasi katika nchi hiyo.
Kwa hakika, Malong anataka aonekane kuwa ndiye
hasa mwenye mamlaka nyuma ya kiti cha Kiir.
Kwa siku kadhaa kumekuwako mivutano katika
mji mkuu wa Juba baina ya wapiganaji
wanaomuunga mkono Machar na wanajeshi wa
Kiir.
Machar aliporejea Juba kutoka mafichoni na
uhamishoni, kama vile mapatano ya amani
yalivyotaka, aliruhusiwa kuwa na wapiganaji wake
2, 000 katika mji huo. Wengi wa askari 10, 000
wa jeshi la Taifa waliwekwa kilomita 25 nje ya mji
huo.
Hali hiyo ilikuwa ya hatari kwa wapiganaji wa
Machar, bila ya shaka. Pale mvutano ulipozidi,
Kiir na Machar walikutana katika Kasri la Rais
kuujadili mzozo huo.
Mtu muhimu aliyekosekana katika mazungumzo
hayo alikuwa Malong, licha ya kwamba kuwako
kwake, kama mkuu wa majeshi, kulikuwa ni
jambo la lazima.
Malongo anaweka kwamba hayatilii maanani
mapatano ya amani yaliofikiwa baina ya Kiir na
Machar. Anahisi Kiir amesalimu amri na
amelegeza kamba katika masuala mengi.
Mkuu huyo wa majeshi anaonekana kama vile
anahisi Sudan Kusini ni mali ya Wadinka, hivyo ni
lazima watu wa kabila hilo wadhibiti nyadhifa
muhimu katika Serikali, siasa na jeshi.
Anapowataja Wadinka anakusudia Wadinka wa
Mkoa wa Bahr el-Ghazal ambako yeye na Kiir
wanatokea na anaowaona kuwa ni bora kuliko
wale wa maeneo mengine ya nchi.
Malong hajapendezwa na Serikali ya mpito
iliyoundwa na ambayo ndani yake kuna watu wa
mkabila mengine pia. Pia, hajavutiwa na wazo la
kuwachanganya wanajeshi pamoja na wapiganaji
wa Machar ili liundwe Jeshi moja la Taifa.
Kabla ya mwaka 2013 Wanuer walikuwa ni
sehemu kubwa jeshini, lakini tangu vita vya
kikabila kuanza Jeshi la Serikali limegeuka kuwa
na Wadinka wengi.
Malong anataka urais
Tetesi zinaenea huko Sudan Kusini kwamba
Malong anajaribu kuwagonganisha Kiir na Machar
ili yeye aje kuwa rais. Kuna watu nchini humo
wanaomuogopa Malong na kuna wale
wanaomtuhumu, japokuwa hamna ushihidi
uliotolewa hadi sasa, kwamba alikuwa dhamana
ya mauaji ya Wanuer katika mji wa Juba pale vita
vya kienyeji vilipoanza mwaka 2013.
Licha ya yote hayo bado haifahamiki nani hasa
aliyesababisha mapigano ya hivi karibuni.
Japokuwa mara hii, kama ilivyokuwa hapo kabla,
jina la Malong limeibuka hapa na pale, lakini
mambo mengi bado si wazi.
Pia mara hii, kama ilivyokuwa miaka mitatu
iliyopita, mapigano haya hajazuka papo kwa
papo. Wakati ule, kama ilivyokuwa mara hii,
lazima kulikuwako mpango ulioandaliwa kabla.
Amani imetoweka
Jambo moja ni hakika, nalo ni kwamba mpango
wa amani wa Sudan Kusini kwa sasa umetupwa
ndani ya pipa la taka. Baada ya kutokea mara hii
mauaji mengine chuki zimeongezeka na hali ya
kutoaminiana imezagaa. Amani kamili kwa sasa
ni ndoto.
Mapigano haya ya karibuni huko Juba
yameirejesha Sudan Kusini ndani ya janga jipya.
Wote wawili, Kiir na makamu wake , Machar,
hawajaijenga na kuipatia maendeleo nchi yao
tangu iliopoata uhuru miaka mitano iliyopita.
Viongozi hao wawili wamejidhihirisha kwamba ni
wababe katika kuendesha vita baina yao. Tatizo
la Sudan Kusini ni tu uchu wa madaraka.
Mahasimu hao wanataka wao na makabila yao
wajilimbikizie madaraka. Jambo la ajabu na
kusikitisha ni kwamba kila mmoja wao anahisi
ana haki miliki ya kuogoza nchi na makabila
mengine yawe mashahidi wa sarakasi yao.
Sumu hii ya ukabila ndiyo kiini cha mzozo wa
Sudan Kusini. Sasa mapatano ya amani
yaliyofikiwa Agosti mwaka jana na yaliyokomesha
vita vya kienyeji vilivyochukuwa maisha ya watu
50, 000 hayana thamani yoyote.
Licha ya kwamba wote wawili, Kiir na Machar,
waliweka alama za vidole vyao katika karatasi za
mkataba huo, lakini kila mtu duniani alianza kuwa
na wasiwasi pale Kiir tangu mwanzo alipoanza
kuukosoa mkataba huo. Ishara ya kukosekana nia
safi ya kuutekeleza mkataba huo ilionekana tangu
mwanzo. Lakini walimwengu, kwa masikitiko,
walilipuuza jambo hilo.
Uchumi umezorota
Licha ya uhasama baina ya Kiir na Machar, Sudan
Kusini ina tatizo jingine kubwa tangu kupata
uhuru, nalo ni la kiuchumi. Japokuwa Sudan
Kusini ina robo tatu ya akiba ya mafuta
yaliokuwako katika ardhi ya Sudan nzima, lakini
Sudan Kusini hiyo inaitegemea Sudan Kaskazini
kuweza kusafirisha mafuta yake kwenda ng’ambo.
Kwa miaka sasa Juba na Khartoum zimekuwa
zikibishana vikali juu ya malipo ya kutumia
mabomba ya kupitishia mafuta kutokea Sudan
Kusini hadi Kaskazini na kuwasili bandarini katika
Bahari ya Sham.
Mara kadhaa kumekuwako mapigano katika
mpaka baina ya Sudan na Sudan Kusini. Pia,
mambo yamekuwa magumu kwa Wasudani Kusini
kutokana na kuporomoka bei ya mafuta katika
masoko ya dunia, maisha kuwa ghali na ufisadi
kuzidi nchini humo.
Suluhisho?
Sudani Kusini itakuwa katika hali bora ikiwa Kiir
na Machar watastaafu na kuchukua pensheni zao.
Lakini isisahaulike kwamba wao ni wawakilishi wa
makabila mawili makubwa katika nchi hiyo.
Ama sivyo inawabidi wajifunze kuishi pamoja na
kuheshimiana. Matarajio yako kwa Umoja wa
Afrika (AU) na nchi zinazoizunguka Sudan, hasa
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Itasikitisha pindi mzozo huu wa Kiafrika
utawachiwa upatiwe ufumbuzi na madola makuu,
nje ya Afrika. Pia, kuna nchi kadhaa duniani
zilizokwenda mbio hapo zamani kuitia moyo
Sudan Kusini ijitenge kutoka Sudan. Inafaa sasa
nchi hizo nazo pia ziende mbio kuhakikisha
Sudan Kusini ina angalau amani.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni