0
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na
Mbunge wa jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga
(CCM) amezungumzia jinsi alivyopokea
kutumbuliwa kwake na Rais John Magufuli
ambaye anaamika kuwa rafiki yake akisema
hawezi kuhoji uamuzi huo.
Kitwanga aliwaaambia waandishi wa habari
nyumbani kwake Misungwi kuwa ingawa hawezi
kuhoji uamuzi huo, kuna kundi kubwa la wauza
madawa ya kulevya ndio waliolikuza tukio hilo
kwa lengo la kumchongea hadi kuondolewa
kwenye nafasi hiyo.
“Anayofanya Dk. Magufuli nampongeza sana
kwani ni mtu ambaye namfahamu. Ni mwadilifu,
msikivu, namshukuru kwa kuniamini kufanya kazi
naye katika Serikali yake hivyo siwezi kuhoji
alichoamua kwa sababau aliyetoa ndiye
aliyeondoa,” alisema Kitwanga.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo wa Misungwi
alikana kuhusika kwa namna yoyote katika sakata
la kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd iliyopewa
zabuni ya kufunga mashine za kutambua alama
za vidole kwenye vituo vya polisi nchini, na
kudaiwa kulipwa kiasi kikubwa cha fedha wakati
kazi haikufanyika kama ilivyotarajiwa. Sakata hilo
bado lipo katika uchunguzi japo dalili za
kujadiliwa bungeni zinaonekana kufifia.
“Rais wa Kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu
Julius Nyerere, kuna wakati alituhumiwa akidaiwa
kuwa na mpango wa kumpindua Rais wa Kenya
baada ya kuzuru nchini humo. Alipoulizwa na
waandishi wa habari alijibu, ‘hivi mtu akikwambia
mimi ni mume wa mama yako utakubali?’, sasa
hilo ndilo jibu langu kwa Watanzania ili
wasiniulize tena,” alisema Kitwanga.
Akizugumzia umiliki wa kampuni ya Infosys,
alisema kuwa yeye ni mwanzilishi tu wa kampuni
hiyo na hivi sasa inamilikiwa na mwanae baada
ya kumuuzia asilimia 33 ya hisa zake na kwamba
taarifa ya mauzo hayo ziko wazi.

Chapisha Maoni

 
Top