0

Mahakama ya Tanzania imeamua kuchukua
juhudi za makusudi ili kubadilisha
muonekano wake na kuwa chombo
kitakachojibu maswali na kuondoa kiu ya
watanzania katika kupata haki kwa
wakati.
Akifungua Mkutano wa Mahakama ya
Tanzania na wadau wake wa kujadili
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa mhimili
huo leo mjini Dodoma, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu kanda ya Dodoma
Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko amesema
Mahakama ya Tanzania inakusudia
kukibadilisha chombo hicho ili kiweze kutoa
haki kwa wakati kwa mujibu wa jukumu
ililopewa na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Alisema katika kufanikisha azma hiyo,
Mahakama ya Tanzania inaendelea na
mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi wake
yanayolenga kuuboresha Mpango Mkakati
wake kwa kushirikiana na wadau ili
kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa
wakati na taswira ya mahakama inakuwa
chanya wakati wote.
Jaji Kwariko amesema Mahakama imeamua
kuwashirikisha wadau kwenye Mpango
Mkakati wake kwa kuwa umuhimu na
nguvu waliyonayo Sitasaidia kufanikisha
utendaji wa Mahakama katika kuyafikia
malengo ya kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Aidha, Jaji Kwariko aliwataka watumishi
wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi
kwa bidii katika kuutekeleza Mpango
Mkakati kwa kuwa utendaji kazi wao
utapimwa kwa jinsi watakavyotekeleza
majukumu yao kulingana na Mpango
Mkakati huo. Aliongeza kuwa Mahakama ya
Tanzania itaelekeza rasilimali zake zote
kama vile watu, fedha na muda katika
kuleta matokeo makubwa yanayotarajiwa.
Alisema endapo watumishi hao watajikita
katika kufanikisha uimara wa nguzo zote
tatu za Mpango Mkakati huo, upatikanaji
wa haki kwa wakati na uhusishwaji wa
wadau na imani ya wananchi vitakifanya
chombo hicho kutimiza ndoto yake na
kuifikia dira yake. Nguzo tatu za Mpango
Mkakati huo ni Utawala bora, Uwajibikaji
na Usimamizi wa rasilimali.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati
alisema baada ya Mpango Mkakati wa
Mahakama kukamilika, watumishi
watasaini kadi itakayokuwa ikionyesha
namna ya utekelezaji wa Mpango Mkakati
na kadi hiyo itaweka alama za kuonyesha
ufaulu katika utekelezaji, endapo mtumishi
atapata alama ndogo atachukuliwa hatua.
Akizungumzia namna Mahakama
inavyopambana na rushwa, Msajili huyo
alisema Mahakama imeweka mazingira ya
uwazi katika utoaji wa huduma zake
pamoja na kuweka mifumo ya kielekitroniki
na kuhusisha wadau wake katika utendaji
kazi wake.
Mahakama ya Tanzania inaendelea na
Mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi wake
kuhusu uandaaji na utekelezaji wa Mpango
Mkakati wake ambapo leo ilikutana na
wadau wake ili kujadili namna ya
utekelezaji wa Mpango huo.
Wadau waliohudhuria, mafunzo hayo leo ni
Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali, Polisi Makao
Makuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa-TAKUKURU na Wakala wa
Majengo Tanzania-TBA.
Wengine ni pamoja na Baraza la Habari
Tanzania-MCT, Tume ya Kurekebisha
Sheria, Tume ya Usuluhishi wa Migogoro,
Ofisi ya Nyaraka za Taifa na Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-
TAMISEMI.



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top