Mvutano wa kisiasa baina ya vijana wa CCM na CHADEMA kuhusu katazo la mikutano ya vyama vya siasa umezidi kukua huku jeshi la polisi
likitarajiwa kutoa tamko kuhusu hali hiyo.
Hali hiyo ya jino kwa jino imejitokeza zikiwa zimebakia siku 16 kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa CCM July 23, ambao Baraza la
Vijana la CHADEMA ( BAVICHA ) limesema
litawasaidia polisi kuuzuia.
Tayari BAVICHA limetangaza kuandaa vijana 5000 kutoka sehemu mbalimbali nchini kwenda kuzuia
mkutano huo utakaotumika kumkabidhi Rais John
Magufuli uenyekiti wa chama hicho.
Jumatatu iliyopita, Kaimu Katibu Mkuu wa
UVCCM, Shaka Hamdu Shaka aliionya Bavicha wasiende Dodoma kuzuia mkutano wa CCM kwa
kuwa watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda
heshima ya chama chao.
Shaka alisema mkutano huo utafanyika kama
ulivyopangwa, hivyo Bavicha kama kweli ni
vidume wa mbegu wajitokeze ili wakione cha mtema kuni.
Shaka alisema UVCCM wako tayari kuidhihirishia dunia kwa kuwatia adabu Bavicha na kuonya
wasijaribu kufanya jambo lolote linalotishia kuhatarisha usalama au ustawi wa maendeleo ya
kisiasa ya CCM kwa saa, siku, wakati na mahali
popote.bShaka aliwataka Bavicha kuacha siasa za
mikwara, vitisho, kutishia usalama na amani ya
nchi kwa kujifanya vijogoo wakati hawana lolote wanaloweza ama kuzuia, kujenga au kubomoa.
Alipoulizwa kuhusu mvutano huo, Msemaji wa
Polisi nchini, Advera Bulimba alisema jeshi hilo litatoa taarifa na ufafanuzi kuhusu zuio la
mikusanyiko ya vyama vya siasa leo.
Sintofahamu ilivyoanza
Utata huo uliibuliwa na amri ya Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo wa Polisi Makao, Nsato
Mssanzya ya kuzuia mikutano na maandamano
yote ya vyama kwa madai kwamba vyanzo vyake
vya kiintelejensia vilibaini kuwapo kwa uwezekano
wa kutokea kwa vurugu.
“Jeshi la polisi nchini linapiga marufuku
maandamano na mikutano yote ya hadhara
kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya
usalama itakapotengamaa." Ilisema sehemu ya
taarifa ya jeshi la polisi
Baada ya katazo hilo, jeshi hilo lilitawanya
mikutano ya ndani ya Chadema, yakiwamo
mahafali ya vijana wa chama hicho (Chaso)
yaliyopangwa kufanyika Dodoma kwa madai ya
kuwapo mlipuko wa ugonjwa usiofahamika.
Hatua hiyo ya polisi ilikuja baada ya Chadema
kutangaza mpango wa kuzunguka nzima kueleza
masaibu ya kidemokrasia yanayokikumba na
baadaye CCM kutangaza kupita katika maeneo
hayo ‘kufuta nyayo”.
Katibu wa Bavicha, Julius Mwita alisema mpaka
jana tayari vijana 5,000 walikuwa wakijiandaa
kwenda Dodoma; “kushirikiana na polisi
kuwafundisha CCM kuheshimu amri zinazotolewa
na viongozi. "
"Tumeandaa vijana 5,000 kutoka mikoa 19 nchini
ambao wamejitolea kwa nauli zao kwenda
Dodoma kushirikiana na jeshi la polisi
kuhakikisha mkutano wa CCM haufanyiki.”
Watembelea Butiama
Katika hatua nyingine, viongozi wa Chadema juzi
walitembelea kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere huko Butiama, wakisema
walikwenda kumshtaki Rais Magufuli kwa
kuminya demokrasia.
Mwenyekiti wa Bavicha, Pastrobas Katambi
alisema chama hicho kinatambua jitihada
zilizofanywa na Mwalimu Nyerere katika kukuza
na kuendeleza ustawi wa jamii ya kidemokrasia
nchini.
“Tunapenda kuwaambia watawala kwamba amani
ni tunda la haki na ni muhimu utawala
ukaheshimu misingi ya kikatiba iliyoachwa na
Baba wa Taifa,” alisema Katambi.
Kauli za CCM, Chadema
Naibu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika
alisema anabariki maandalizi ya mpango na
kitendo kinachotarajiwa kufanywa na Bavicha ili
kuwepo na usawa wa kidemokrasia.
“Kama ni ruhusa iwe kwa wote na kama zuio liwe
kwa wote, haina maana Chadema wazuiwe lakini
CCM waendelee na mikutano yao ya kisiasa,”
alisema Mnyika.
Kaimu Katibu wa CCM, Mkoa wa Dodoma alisema
mkutano huo ni wa kitaifa na wala si wa mkoa na
kushauri atafutwe Msemaji wa CCM, Christopher
Ole Sendeka.
“Sisi tunatekeleza maagizo tunayopewa na si
vinginevyo,” alisema. Ole Sendeka hakupatikana
na simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa alisema mkutano wa CCM ni wa
ndani wala hakuna tatizo lolote kwa kuwa
mikutano ya ndani inaruhusiwa na kuwa jeshi hilo
litawalinda wanaCCM.
Kuhusu Jeshi hilo kuzuia mikutano ya Chadema,
Mambosasa alisema walizuia bendera na si
vinginevyo na kuwa alitoa taarifa ikiwa kamili
lakini waandishi walipotosha.
Manyara wajiandaa
Zaidi ya vijana 560 wa Mkoa wa Manyara,
wamejiandikisha tayari kuelekea Dodoma kwa ajili
ya kuwasaidia polisi kuzuia mkutano wa CCM ili
kuunga mkono agizo la kupigwa marufuku
mikusanyiko ya kisiasa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Manyara, Francis Massawe aliwataka vijana hao
kuachana na mpango huo wa kitoto kwani wao
wamejipanga kushughulika na watu wanaotaka
kuanzisha vurugu.
Kamanda Massawe alisema endapo kuna kundi
linataka kukwamisha mkutano halali wa CCM wa
kumchagua mwenyekiti wao, wasubiri hadi
mwaka 2020 ndipo wafanye na kwamba polisi
hawatakubali hilo litokee.
“Hao vijana wanacheza ngoma ya kitoto ambayo
haikeshi kwani wanaingilia majukumu ambayo
siyo yao, uchaguzi wa CCM hauna ubishi lazima
ufanyike na hakuna wa kuzuia, hao wanacheza
kombolela,” alisema.
Msimamo wa Zitto
Akizungumzia uamuzi wa Bavicha, Kiongozi wa
ACT Wazalendo ambacho pia mitano yake
imezuiwa, Zitto Kabwe alisema haoni tatizo
kuhusu suala hilo kwa kuwa wanafanya siasa,
hivyo haoni kama ni njia mbaya.
Zitto alisema chama chake hakiwezi kusema moja
kwa moja kuwa kinaunga mkono uamuzi wa
Bavicha lakini wao watakwenda mahakamani
kupinga hatua ya Serikali kuzuia uhuru wa vyama
vya siasa kufanya mikutano yao.
Chapisha Maoni