0
Maafisa watano wa polisi mjini Dallas, Marekani
wamepigwa risasi na kuuawa wakati wa
maandamano ya kupinga mauaji ya watu weusi.
Maafisa wengine sita wanauguza majeraha.
Maafisa wa polisi katika mji ulio katika jimbo la
Texas, wanasema mauaji hayo yametekelezwa na
washambuliaji wawili wa kulenga shabaha.
Mkuu wa polisi wa Dallas David Brown amesema
amesema maafisa wa polisi bado wanakabiliana na
mshukiwa mmoja ambaye anadaiwa kujibanza
katika jumba linalotumiwa kuegesha magari.
“Mshukiwa huyo ambaye tunawasiliana naye
amewaambia maafisa wetu kwamba mwisho
unakaribia na kwamba ataumiza na kuua wenzetu
wengi, akimaanisha maafisa wa usalama na
kwamba kuna mabomu yaliyotegwa eneo lote,
kwenye gereji na katikati mwa jiji.”
Vyombo vya habari jimbo hilo vinasema
kumetokea mlipuko mkubwa eneo hilo lakini habari
hizo hazijathibitishwa.
Mtu mweusi Sterling alivyouawa Marekani
Bw Brown amesema mwanamke aliyekuwa karibu
na eneo alimojificha mwanamume huyo anahojiwa
na maafisa wa usalama.
“Hatuwezi kusema kwamba tumewakamata
washukiwa wote,” alisema mkuu huyo wa polisi.
Ufyatuaji risasi ulitokea mwendo wa saa tatu
kasorobo usiku saa za Texas waandamanaji
walipokuwa wakipitia barabara za mji na
kuwafanya waandamanaji kukimbilia usalama wao.
Maandamano hayo yalitokana na kuuawa kwa
wanaume wawili weusi, Philando Castile jimbo la
Minnesota na Alton Sterling eneo la Baton Rouge
jimbo la Louisiana.
Miongoni mwa maafisa wa polisi waliofariki ni afisa
wa trafiki Brent Thompson, 43.
Donald Trump anusurika kuuawa
Raia mmoja, ambaye jamaa zake wamesema jina
lake ni Shetamia Taylor, alipigwa risasi mguuni
akiwakinga watoto wake na kwa sasa anapokea
matibabu hospitalini.
Meya wa Dallas Mike Rawlings amesema "huu ni
wakati wa kusikitisha sana kwa jiji letu.”
Rais wa Marekani Barack Obama, akirejelea
takwimu zinazoonesha kwamba kuna uwezekano
mkubwa wa Wamarekani Weusi kupigwa risasi na
maafisa wa polisi kuliko Wamarekani Wazungu,
amesema ubaguzi huo unafaa kumalizwa.
"Visa kama hivi vinapotokea, kuna sehemu kubwa
ya raia wanaohisi kwamba kwa hawatendewi haki
kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, kwa sababu
hawatazamwi kwa njia sawa. Na hili linauma,”
amesema.
Takwimu kutoka kwa shirika linalotetea maafisa wa
polisi Marekani la Officer Down Memorial
zinaonesha maafisa 53 wa polisi wameuawa
wakiwa kazini mwaka 2016, 21 wakiuawa kwa
kupigwa risasi. Idadi hiyo haijumuishi maafisa
waliouawa Dallas.

BBC

Chapisha Maoni

 
Top