John Pombe Magufuli amewahakikishia
wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar
es salaam ni salama kwa wao kupitisha mizigo na
ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea
kuchukua hatua za kuiboresha bandari hiyo na
kurahisisha biashara kati ya nchi hizi mbili.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01
Julai, 2016 alipokuwa akizungumza na wananchi
wa Tanzania na Rwanda kupitia vyombo vya
habari wakati wa ziara rasmi ya kiserikali ya Rais
wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame
inayofanyika kwa siku mbili hapa nchini.
Dkt. Magufuli amesema pamoja na kuchukua
hatua kadhaa za kuboresha bandari ya Dar es
salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara
wanaopitisha mizigo, Tanzania imeamua kuipatia
Rwanda eneo la kujenga bandari kavu kwa ajili ya
mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA) itafungua ofisi Mjini
Kigali nchini Rwanda ikiwa ni juhudi za
kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi
hizi mbili.
Aidha, Rais Magufuli amesema kwa kutambua
umuhimu wa reli ya kati kwa uchumi wa Tanzania
na Rwanda, Tanzania imetenga shilingi Trilioni
moja katika bajeti mpya ya serikali kwa ajili ya
kuanza ujenzi wa Reli hiyo kwa kiwango cha
kisasa yaani “Standard Gauge” na kwamba ni
matarajio kuwa wadau wengine wa maendeleo
watajitokeza kuunga mkono juhudi za ujenzi wa
reli hiyo hapa Tanzania na nchini Rwanda huku
akidokeza kuwa China imeonesha nia ya kuunga
mkono mradi huo.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa serikali yake pia
imechukua hatua madhubuti za kulifufua shirika
la ndege la Taifa na kwamba tayari mipango
imefanywa kuhakikisha ndege mbili aina
Bombadier Q400 zinanunuliwa na zitatua hapa
nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba
Mwaka huu 2016.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda
Mhe. Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli
kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali
hapa nchini na amemhakikishia kuwa serikali
yake itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano
uliopo kati ya nchi yake na Tanzania kwa
manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Majira ya jioni Rais Kagame akiwa na mwenyeji
wake Rais Magufuli, amefungua rasmi maonesho
ya 40 ya kimataifa ya Biashara Dar es salaam
yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba
vilivyopo Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke,
Mkoani Dar es salaam.
Akizungumza kabla ya kuzindua rasmi maonesho
hayo, Rais Kagame ametoa wito kwa Tanzania na
Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya
Afrika Mashariki kushirikiana na sekta binafsi
katika kutumia fursa nyingi za kibiashara zilizopo
baina yake na kuwaletea manufaa wananchi.
Nae Rais Magufuli amezipongeza nchi takribani
30 zilizojitokeza kushiriki katika maadhimisho
hayo zikiwemo kampuni zaidi ya 650 na wadau
zaidi ya 2,000 na amesisitiza umuhimu wa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
zenye watu takribani milioni 165 na nchi nyingine
za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika
(SADC) kuongeza biashara baina yake kwa kuwa
hivi sasa kiwango cha biashara baina ya nchi
hizo ni cha chini mno.
Baada ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame
na mwenyeji wake Rais Magufuli wametembelea
mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa na
huduma katika viwanja vya Sabasaba na baadaye
Rais Kagame atahudhuria dhifa ya Kitaifa
iliyoandaliwa na mwenyekiji wake Rais John
Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
01 Julai, 2016

Chapisha Maoni