0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt John Pombe Magufuli akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa
Dodoma mapema leo asubuhi waliojitokeza kushuhudia maadhimisho ya Siku ya
Kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.PICHA NA MICHUZI JR-DODOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewasihi watanzania kuwaenzi
Mashujaa kwa kudumisha Amani, Umoja
na Utulivu uliojengwa na mashujaa
hao.Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo
tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa
maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya
Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja
wa Mashujaa Mjini Dodoma.
Pamoja na kutoa rai hiyo Rais Magufuli
ameahidi kuwa atahakikisha azma ya
Serikali kuhamia Dodoma inatekelezwa
kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha
uongozi wa miaka mitano.
"Tunapoadhimisha siku ya Mashujaa
hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba
wa Taifa alisema makao makuu yawe
Dodoma, haiwezekani sisi watoto wake, sisi
wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.
"Kwa hiyo nilikwishazungumza na leo
narudia hili katika siku ya Mashujaa,
mlinichagua ndugu zangu wa Dodoma kwa
kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi
minane imepita, nimebakiza miaka minne
na miezi minne, nataka kuwathibitishia
kuwa katika kipindi cha miaka minne na
miezi minne iliyobaki nitahakikisha serikali
yangu pamoja na mimi tunahamia Dodoma
bila kukosa" Amesema Rais Magufuli.
Kufuatia maelekezo hayo ya Mhe. Rais,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
ameagiza Mawaziri wote waanze mara
moja kuhamia Dodoma na kwamba yeye
mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma
ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Viongozi wengine waliohudhuria
maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali
Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama
Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Tulia Ackson, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid,
Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John
Samwel Malecela na Mhe. Mizengo
Kayanza Peter Pinda, Mabalozi na
wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali,
Viongozi wa vyombo vya ulinzi na
usalama, Viongozi wa vyama vya siasa na
dini, maafisa na askari waliopigana vita
mbalimbali.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU Dodoma
25 Julai, 2016



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top