Ndugu John Pombe Joseph Magufuli
alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 katika
kijiji cha Chato, Wilayani Biharamulo katika
Mkoa wa Kagera. Hivi sasa Chato ni Wilaya
katika Mkoa wa Geita. Ndugu Magufuli ni
Daktari wa Falsafa (PhD) ya Kemia. Ana
mke na watoto saba. Alichaguliwa kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mwezi Oktoba, 2015 kwa tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (C.C.M). Aliapishwa na
kuanza rasmi majukumu yake ya kuiongoza
Tanzania tarehe 5 Novemba, 2015.
Tangu ameingia madarakani, Rais Dkt.
Magufuli, ameonesha kuwa ana sifa zote
muhimu za uongozi. Ana dira, maono na
malengo kuhusu anakotaka Taifa liende.
Ana mikakati ya kutekeleza dira na maono
yake. Haogopi kufanya maamuzi makini.
Ana kiu ya kuona Taifa linapata maendeleo.
Amejipambanua kuwa yeye ni mtetezi wa
wanyonge na dhamira yake kubwa ni kuona
wananchi wanapata huduma bora za jamii
na kero zao zinaondoka.
2.0. ELIMU NA MAFUNZO
Rais Dkt. Magufuli alianza elimu ya msingi
katika Shule ya msingi Chato mwaka 1967
na kumaliza mwaka 1974. Mwaka 1975
alianza masomo ya sekondari katika Shule
ya Seminari ya Katoke Mkoani Kagera.
Mwaka 1977 alihamia shule ya sekondari ya
Lake iliyopo Mkoani Mwanza na kuhitimu
kidato cha Nne mwaka 1978. Kuanzia mwaka
1979 hadi 1981 alifanya masomo ya kidato
cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari
ya Mkwawa Mkoa wa Iringa .
Mwaka 1981 hadi 1982 alisoma Chuo cha
Ualimu Mkwawa na kuhitimu Stashahada ya
Ualimu ya Masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwezi Julai hadi Disemba mwaka 1983, Dkt.
Magufuli alipata mafunzo ya kijeshi katika
Jeshi la kujenga Taifa kikosi cha
Makutupora mkoa wa Dodoma. Mwezi
Januari hadi Machi 1984 alihamishiwa
kikosi cha mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa
Makuyuni, Arusha. Mwezi huo wa Machi
alihamia kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa
Mpwapwa Dodoma na kumaliza mafunzo
mwezi Juni 1984.
Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha
Dar es salaam kusoma Shahada ya kwanza
ya Sayansi na Ualimu akijikita katika
masomo ya Kemia na Hisabati. Alitunukiwa
Shahada hiyo mwaka 1988. Mwaka 1991
hadi 1994 alisoma na kutunukiwa Shahada
ya Uzamili katika fani ya Kemia iliyotolewa
na Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo
Kikuu cha Salford cha Uingereza. Mwaka
2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kwa ajili ya Shahada ya Uzamivu
katika Fani ya Kemia na kufanikiwa
kuhitimu mwaka 2009.
3.0. UZOEFU WA NDANI YA SERIKALI
Baada ya kuhitimu masomo yake ya
Stashahada ya Ualimu, mwaka 1982 hadi
1983 Dkt. Magufuli alikuwa Mwalimu katika
shule ya Sekondari ya Sengerema iliyopo
Mkoani Mwanza akifundisha masomo ya
Kemia na Hisabati. Mwaka 1989 alijiunga
na Chama Cha Ushirika cha Nyanza Mkoani
Mwanza, ambapo alifanya kazi kama
Mkemia Mkuu hadi mwaka 1995.
Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa
Jimbo la Biharamulo Mashariki Mkoa wa
Kagera. Baada ya Uchaguzi, Rais wa
Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin
William Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri
wa Wizara ya Ujenzi nafasi ambayo
aliitumikia hadi mwaka 2000. Mwaka 2000
alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge
wa Jimbo la Biharamulo Mashariki lakini
mara hii akipita bila kupingwa. Mwaka huo
huo aliteuliwa kuwa Waziri kamili wa
Wizara ya Ujenzi hadi mwaka 2005.
Mwaka 2005 Rais Dkt. Magufuli alichaguliwa
kwa mara ya tatu kuwa mbunge wa jimbo la
Biharamulo Mashariki, kwa mara nyingine
akipita bila kupingwa. Baada ya uchaguzi,
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008
ambapo alihamishiwa Wizara ya Mifugo
na Maendeleo ya Uvuvi hadi hadi mwaka
2010.
Mwaka 2010 Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa
mara ya nne kuwa Mbunge lakini, kufuatia
mgawanyo wa majimbo uliofanyika, mara
hii katika Jimbo jipya la Chato. Baada ya
uchaguzi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi
kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Wakati akiwa Mbunge na Waziri, Dkt.
Magufuli amefanya shughuli na kushika
nyadhifa kadhaa ndani na nje ya nchi.
Mwaka 2014, Dkt. Magufuli alishiriki katika
Bunge Maalum la Kutunga Katiba Mpya
akiwa ni Mjumbe wa Bunge hilo. Aidha,
wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi aliweza kuchaguliwa
kuwa Mwenyekiti Mwenza (Co-Chair) wa
Mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat).
Tarehe 25 Oktoba, 2015 Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli alichaguliwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
tarehe 5 Novemba, 2015 aliapishwa kushika
rasmi wadhifa huo.
4.0. UZOEFU WA UONGOZI NDANI YA
CHAMA
Rais Dkt. Magufuli alijiunga na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mwaka 1977. Amekuwa
Mwanachama mwaminifu na ameshika
nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya
Chama. Nafasi alizowahi kushika ni pamoja
na kuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya
Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
CCM Wilaya, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Mkoa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa
na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Sambamba na kushika nafasi mbalimbali za
uongozi, Dkt. Magufuli mara zote alijitoa
kukitetea Chama na kuhakikisha kinapata
ushindi. Alishiriki kikamilifu kuwafanyia
kampeni wagombea wa CCM katika Chaguzi
Ndogo zilizofayika katika majimbo ya
Busanda, Biharamulo Magharibi na Igunga
na kupata ushindi. Katika Mkutano Mkuu
wa CCM wa tarehe 11 – 12 Novemba mwaka
2012, Dkt. Magufuli alikuwa miongoni mwa
Mawaziri wachache waliopata fursa ya
kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya Chama ya Mwaka 2010 –
2015. Alielezea mafanikio ya utekelezaji wa
Ilani, hususan katika sekta ya
miundombinu.
Tarehe 11 mwezi Julai, 2015 Mkutano Mkuu
wa Taifa wa CCM ulimchagua na kumteua
Dkt. Magufuli kuwa mgombea Urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliinadi vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM
(2015) na kukiwezesha Chama kupata
ushindi mkubwa. Tarehe 25 Oktoba, 2015
alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Nafasi hiyo
imemwezesha kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa.
5.0. UFANISI KATIKA UONGOZI
Dkt. Magufuli ni kiongozi mnyenyekevu, aliye
na hofu ya Mungu, mkweli, mtekelezaji wa
ahadi, mwadilifu, shupavu, mahiri,
mbunifu, mtafiti, mchapakazi na mtetezi wa
wanyonge. Ni kiongozi mpenda haki na
mchukia dhuluma, rushwa, ufisadi na
ubaguzi wa aina yoyote ile. Ni kiongozi
mwenye msimamo na mtetezi wa yale
anayoyaamini.
Katika nyadhifa zote alizopata kutumikia
alifanya kazi kwa uadilifu na umahiri
mkubwa. Amejidhihirisha na kujipambanua
kuwa ni mfuatiliaji na msimamizi wa
sheria. Akiwa Mwalimu Sengerema
Sekondari aliwezesha wanafunzi wote wa
darasa lake kufaulu masomo ya Hesabu na
Kemia aliyokuwa akiyafundisha. Akiwa
Mkemia Mkuu wa Chama cha Ushirika cha
Nyanza alisimamia vyema ubora wa
uzalishaji wa mafuta ya Pamba na kuifanya
Kampuni ya Nyanza kuwa mzalishaji mzuri
wa mafuta ya Pamba.
Akiwa Waziri wa Ujenzi anakumbukwa kwa
kubuni na kusanifu miradi ya ujenzi wa
barabara, kusimamia vizuri matumizi ya
fedha na kuhakikisha miradi hiyo
inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati
uliopangwa. Uwezo wake katika kubuni na
kusanifu miradi ya barabara uliigwa na
nchi majirani, ikiwemo Kenya. Ameondoka
Wizara ya Ujenzi akiwa amesimamia ujenzi
wa zaidi ya Kilometa 17,000 za barabara za
lami, madaraja makubwa zaidi ya 14 na
madaraja madogo madogo zaidi ya 7,000 na
vivuko. Aidha, alisimamia vizuri taasisi
mbalimbali za Makandarasi, Wahandisi,
Wabunifu na Wakadiriaji Majengo.
Dkt. Magufuli pia anasifika kwa uwezo wake
mkubwa wa kuweka kumbukumbu ya kazi
zake. Akiwa Wizara ya Ujenzi aliweza
kutaja majina ya barabara zilizojengwa au
zilizokuwa katika hatua za ujenzi, urefu
wake, majina ya wakandarasi pamoja na
gharama za ujenzi bila kusoma mahali
popote. Wakati wa Rais Mstaafu Benjamini
William Mkapa alimwita “Askari wa
Mwavuli”.
Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi alisimamia upimaji
wa ardhi za vijiji na viwanja vya makazi, na
kushughulikia migogoro mingi ya ardhi
iliyowahusu wananchi wa maisha ya chini.
Wakati akiwa Waziri wa Wizara ya Mifugo
na Maendeleo ya Uvuvi alikuwa maarufu wa
kutambua na kutaja idadi ya mifugo, kama
vile samaki, ngómbe, mbuzi, kondoo, kuku,
mbwa n.k. Kitendo cha kukamata meli ya
kichina iliyokuwa ikivua samaki kwa wizi
ndani ya Bahari Kuu ya Hindi eneo la
Tanzania kilidhihirisha uzalendo kwa Taifa
lake. Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt.
Kikwete alimpachika jina maarufu la
“Tingatinga”.
Sifa hizi nzuri ameendelea nazo hata baada
ya kuchaguliwa kuwa Rais. Katika miezi
michache ya uongozi wake amethibitisha
anatekeleza ahadi. Aliahidi kutoa elimu bila
malipo na kuanzisha Mahakama ya
Mafisadi. Ameweza kusimamia nidhamu
kwenye utumishi wa umma kwa kuondoa
watumishi hewa na kuchukua hatua dhidi ya
watumishi wa umma wasio waaminifu,
wala rushwa, wazembe na wanaoshindwa
kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Ameweza kudhibiti matumizi mabaya ya
fedha za umma na kuongeza ukusanyaji wa
mapato ya Serikali. Kwa hakika Dkt.
Magufuli anaakisi uongozi bora unaopaswa
kuigwa na viongozi wengi Barani Afrika na
Dunia.
6.0. DHIMA YA UONGOZI WA SERIKALI YA
AWAMU YA TANO 2015 – 2020) NA MALENGO
YAKE MAHSUSI
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 –
2020 inazielekeza serikali zake kutumia
nguvu zake zote kuendelea kupambana na
changamoto kubwa nne;- Kwanza kuondoa
umaskini, Pili, kupunguza tatizo la ukosefu
wa ajira hasa kwa vijana, Tatu, kuendeleza
vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa
mali ya umma, na Nne, kuendelea
kudumisha amani, ulinzi na usalama wa
maisha ya Watanzania na mali zao.
Sambamba na kutekeleza mambo hayo
makubwa manne, kipindi cha Kampeni na
wakati akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba,
2015 Rais Dkt. Magufuli alitaja malengo
mahsusi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Malengo hayo ni haya yafuatayo:
· Kudumisha Muungano, Amani na Umoja
wa Tanzania. Serikali haitamwonea aibu
mtu mwenye nia ya kuvunja Muungano na
kuvuruga amani na mshikamano katika
nchi. Hili alilidhihirisha vizuri wakati wa
uchaguzi wa marudio huko Zanzibar, kwani
Uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu.
· Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kufikia
azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati
kulingana na malengo ya Dira ya Maendeleo
ya Taifa 2025. Viwanda vinalengwa ni
vyenye kutumia nguvu kazi kubwa,
malighafi za ndani ya nchi, kuzalisha
bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya
nchi. Nia ni kukabiliana na tatizo la ajira
na umasikini;
· Kuongeza kasi ya ujenzi wa
miundombinu ya kiuchumi, hususan
miundombinu ya usafiri na nishati;
· Kuimarisha huduma za jamii, hususan
elimu, Afya na Maji. Lengo ni kuhakikisha
huduma hizo zinapatakana sio tu kwa
urahisi bali pia kwa ubora unaostahili ili
kukabiliana na maadui ujinga, umaskini na
maradhi;
· Kusimamia uwajibikaji wa utumishi wa
umma na kuondoa urasimu ndani ya
Serikali. Lengo ni kuhakikisha watumishi wa
umma wanafanya kazi kwa ueledi, uadilifu
na kujituma ili kuwawezesha wananchi
kupata huduma kwa wakati;
· Kuimarisha usimamizi wa rasilimali za
nchi, ikiwemo kuhifadhi mazingira na
kuzidisha vita dhidi ya ujangili. Lengo ni
kuhakikisha rasilimali za nchi
zinawanufaisha watu wote wa kizazi cha
sasa na kijacho. Aidha, ukusanyaji wa
mapato ya Serikali na udhibiti wa matumizi
ya Serikali nao utaimarishwa;
· Kusimamia utawala bora unaozingatia
sheria na haki za binadamu. Jitihada za
makusudi zitaelekezwa katika kuzidisha
mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi,
dhuluma na uonevu wa aina yoyote. Aidha,
maslahi ya makundi mbalimbali katika
jamii, ikiwemo wanawake, wazee, watu
wenye ulemavu na watoto yatalindwa. Kwa
upande mwingine, wananchi watahimizwa
kuheshimu na kufuata sheria za nchi;
· Kulinda usalama wa raia na mali zao
kwa kupambana na uhalifu, ikiwemo wizi,
ujambazi, tatizo la dawa za kulevya n.k.
· Kudumisha na kuendeleza ujirani
mwema, mahusiano mema na Mataifa
mengine duniani pamoja na Mashirika ya
Kimataifa na Kikanda;
· Kuendeleza na kusimamia vizuri
shughuli za michezo, sanaa, burudani na
utamaduni, ikiwemo kukuza lugha ya
Kiswahili.
HITIMISHO
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria
kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya
kiuchumi na kuwataka watanzania
washiriki kufanya kazi kwa bidii na
maarifa ndani ya falsafa ya HAPA KAZI TU.
Dhamira hii inakusudia kuwezesha Taifa
letu kufikia Uchumi wa Kati uaoongozwa na
Viwanda ili kutimiza malengo ya Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni