Kocha Mkuu wa Azam Fc, Zeben Hernandez
amesema anachoangalia kwa sasa ni ushindi dhidi
ya Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii na wala
hafikirii mechi yake ya kirafiki dhidi ya URA ya
Uganda itakayochezwa kesho.
Azam inatarajiwa kujipima na URA kwenye uwanja
wa Azam Complex Chamazi kujiandaa na mechi ya
Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Agosti 17 mwaka
huu, ikiwa ni mechi ya kuzindua msimu mpya wa
Ligi Kuu unaotarajiwa kuanza Agosti 20.
“Naandaa timu ili kuwa na kiwango bora kwa ajili
ya mechi dhidi ya Yanga baada ya kucheza nao
tutaendelea na mfumo ule ule tulioanza nao wa
kuboresha timu ili iweze kuwa bora zaidi hapo
baadaye,”alisema kwenye tovuti ya Azam jana.
URA, ambayo ipo kwenye maandalizi ya msimu
mpya wa Ligi Kuu ya Uganda ni kipimo kizuri kwa
Azam FC kutokana na timu hiyo kumaliza kwenye
nafasi ya tano msimu uliopita ikijikusanyia pointi
47, pointi 10 nyuma ya mabingwa KCCA.
Hiyo itakuwa ni mechi ya nane ya kirafiki kwa
Azam FC katika kujiandaa vema na msimu ujao
ambapo katika mechi saba zilizopita ilishinda
mechi tano na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya
JKT Ruvu na Ruvu Shooting.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, huo ndio utakuwa
mchezo wa mwisho wa kirafiki kwa Azam FC kabla
ya kuanza mikikimikiki ya msimu ujao, wakianza
kucheza dhidi ya Yanga Agosti 17 mwaka huu
katika mechi ya Ngao ya Jamii inayofungua msimu
mpya.
Hata hivyo, Azam imepoteza mechi za ngao ya
Jamii dhidi ya Yanga karibu mara mbili ambapo
zote ilifungwa kwa mikwaju ya penalti.
Posted: 👉👉 ⚽ Africa News Sports
Chapisha Maoni