Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm
amewatuliza wanachama na wapenzi wa timu hiyo
kutokata tamaa baada ya timu yao kupoteza
Kombe la Ngao ya Jamii kwa kufungwa na Azam
juzi.
Yanga ilifungwa kwa mikwaju ya penalti 4-1 katika
mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa
Dar es Salaam.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu bara walikuwa mbele
kwa mabao 2-0 yaliyopatikana kipindi cha kwanza
kupitia kwa mshambuliaji wao Donald Ngoma
kabla Azam haijasawazisha mabao hayo katika
dakika ya 75 na 90 yaliyofungwa na John Bocco
na Shomari Kapombe na hivyo mechi hiyo kwenda
kwenye kupigiana mikwaju ya penalti.
Kulingana na mahojiano aliyofanya na gazeti la
HabariLeo, Pluijm alisema kupoteza taji hilo
haimaanishi kwamba watashindwa kutetea mataji
yao mengine. Yanga inashikilia taji la Ligi Kuu na
lile la Kombe la Shirikisho la TFF (FA).
“Mechi ya jana (juzi) ushindani ulikuwa mkali
sana, wenzetu walituzidi kwenye penalti
wakatufunga, lakini timu yangu pia haikucheza
vibaya,” alisema.
“Lakini wachezaji wangu hawajapumzika vya
kutosha kama ilivyo wa timu nyingine kutokana na
kushiriki kwenye mashindano, hilo nalo pia
limechangia maana ni wachovu,” alisema.
Yanga ipo hatua ya makundi ya michuano ya
Kombe la Shirikisho Afrika na keshokutwa
inatarajiwa kukamilisha ratiba kwa kumenyana na
TP Mazembe ya Congo DR mjini Lubumbashi.
“Lakini kufungwa na Azam sio kwamba
tutashindwa kutetea mataji yetu mengine, timu
yangu bado nzuri na nina uhakika wa kufanya
vizuri kwenye kutetea mataji tunayoyashikilia,”
alisema Pluijm.
Aidha alisema ataitumia mechi na Mazembe
kufanya maandalizi yake ya mwisho kabla ya
kuanza mechi za ligi.
Yanga itaanza mechi yake ya kwanza ya kutetea
taji la Ligi Kuu Agosti 27 ambapo itacheza na JKT
Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
“Tukirudi tutajua namna ya kufanya na makosa
yaliyotokea kwenye mechi ya Azam tutayafanyia
kazi na Mazembe,” alisema.
Like Page ya Facebook Africa Newss Sports Posted: ⚽ Africa News Sports2
Chapisha Maoni