0

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji
amekata kiu ya kile ambacho wanachama wengi na
wapenda soka nchini walikuwa wakikisubiri
kwenye mkutano wa dharura aliouitisha.
Baada ya kujadili, wanachama wa Yanga pamoja
na wajumbe wa bodi wamepitisha kumkodisha
Manji klabu ya Yanga kwa kipindi cha miaka kumi.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa
Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Manji
amesema amepeleka ombi la kuikodisha Yanga
kwa miaka 10.
“Nitaikodisha kwa asilimia 75 na 25 inabaki kwa
wanachama. Nataka kuikodisha timu na nembo,
majengo ya klabu yanabaki kuwa mali ya
wanachama.
“Katika miaka 10, ikipatikana faida 25 inakwenda
kwa wanachama na klabu na 75 kwangu. Kama
itakuwa ni hasara basi inakuwa hasara yangu,
hakuna hasara upande wa wanachama au klabu,”
alisema.
“Tayari nimewasilisha ombi hilo Bodi ya
Wadhamini ambao wao watazungumza na nyinyi
wanachama na kama kutakuwa na makubaliano
basi tutaingia mkataba,” alisema Manji.
Manji alisema masuala ya timu kuhusu usajili,
mishahara, uendeshaji kama safari na gharama
nyingine zitakuwa chini yake.
Pia asilimia 25 ambayo itakuwa ni ya klabu, ndiyo
itatumika kuujenga Uwanja wa Kaunda na Yanga
itakuwa na uwanja wa kufanyia mazoezi na
ikiwezekana hata kuchezea mechi.
Mabadiliko hayo yanakuja siku chache baada ya
mahasimu wa Yanga, Simba kufanya mabadiliko
ambayo yatapelekea Bilionea Mohammed Dewji
kumiliki hisa nyingi katika klabu hiyo.
Aidha katika mkutano huo wa dharura, Wanachama
wa Yanga wamepitisha kwa pamoja kufutwa kwa
uanachama kwa wajumbe watatu wa kamati ya
utendaji.
Waliofutwa uanachama ni Ayoub Nyenzi, Salum
Mkemi na Hashimu Abdallah.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amewaambia
wanachama wa Yanga kwenye mkutano kwamba
hana imani nao.
Uamuzi wa kuvuliwa uanachama ulifikiwa baada ya
wanachama kupiga kura.



Posted: 👉👉 ⚽ Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top