Mabosi wa Yanga wamekiangalia kikosi chao na
kutikisa kichwa wakishindwa kuelewa kitu gani
kilichoikumba hata ikawa jamvi la wageni kwenye
mechi za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika,
lakini wakaamua kufanya jambo moja la maana.
Kwa vile wanajua kuwa mwakani, pia
wataiwakilisha tena Tanzania kwenye michuano ya
kimataifa kwa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika,
mabosi hao wameona isiwe tabu kwa kuamua
kufanya kweli kwa kusajili nyota wawili wapya
kutoka Ghana.
Nyota hao wanaichezea Medeama ambayo iliitoa
nishai Yanga hivi karibuni kwa kuifunga mabao
3-1 katika mechi ya Kombe la Shirikisho, ambalo
nafasi ya Yanga kutinga nusu fainali ni ndogo kwa
pointi ilizonazo katika kundi hilo.
Hata hivyo wakati Yanga ikijiuliza kwanini imefanya
vibaya katika hatua hiyo, mabosi wa juu wa klabu
hiyo tayari wameonyesha nia ya kuwasajili kiungo
Kwame Boahene na mshambuliaji Abbas
Mohammed kutoka Medeama.
Kigogo mmoja wa Medeama ameliambia gazeti la
Mwanaspoti kuwa mabingwa hao wa kihistoria wa
Ligi Kuu Bara wameonyesha nia hiyo japo bado
hawajaweka ofa ya fedha mezani ili kukamilisha
biashara hiyo huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni
mkanganyiko wa nani akatwe klabuni hapo
kuwapisha Waghana hao.
“Yanga imeonyesha nia kwa wachezaji wetu wawili
Kwame Boahene na Abbas Mohammed na
wameahidi kuleta maombi maalum, sisi hatuna
shida kama timu tunapenda kufanya biashara ya
wachezaji,” alisema kigogo huyo.
Ofisa Habari wa Medeama, Patrick Akoto alisema
wanafurahi kuweza kumuuza Enock Agyei kwenda
Azam na sasa wanasubiri kuona kama Yanga
wataleta ofa kwa nyota hao wawili ambao mpaka
sasa wana taarifa za chini chini kuwa wanahitajika.
“Yanga haijaleta ofa yoyote mpaka sasa, ila tuna
taarifa kuwa wameonyesha nia kwa baadhi ya
wachezaji wetu, wakija sisi hatuna tatizo, Rais wa
timu yetu anapenda kufanya biashara,” alisema
Akoto.
“Kwa sasa tunafurahi kusema kuwa dili la Enock
Agyei kwenda Azam limekamilika na tunamtakia
kila la kheri katika maisha yake mapya,” aliongeza
ofisa habari huyo.
Posted: 👉👉 ⚽ Africa News Sports
Chapisha Maoni