0
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba SC kwa mara ya tatu, safari hii akitoka SC Villa ya kwao, Kampala.
Mfadhili wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji ndiye amefanikisha dili la Okwi kurejea Simba na akasema hiyo zawadi yake kwa wapenzi na wanachama wa timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, huku pia akiwatakia Eid Mubarak.
Na Okwi akatiliana saini mkataba wa kujiunga na Simba tena na Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ Jumapili jioni Dar es Salaam.
Okwi aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 alirudi SC Villa kwa mara ya tatu pia mapema mwaka huu kufuatia kuvunja mkataba na klabu ya Sonderjyske ya Denmark aliyojiunga nayo Julai mwaka juzi, baada ya kuona hapati nafasi ya kucheza.
Emmanuel Okwi (kushoto) akisaini mkataba wa kujiunga tena na Simba na Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange 'Kaburu '
Ikumbukwe Okwi alijiunga na SonderjyskE FC ya Ligi Kuu ya Denmark Julai mwaka 2015 akisaini mkataba wa miaka mitano kutoka Simba SC, ambao ulitarajiwa kumalizika mwaka 2020.
Okwi aliyeifungia mabao 18 timu ya taifa ya Uganda katika mechi 35, aliondoka Simba SC baada ya nusu msimu tu tangu arejee kutokea kwa mahasimu, Yanga SC ambako pia alicheza kwa nusu mwaka kabla ya kutofautiana na viongozi wa klabu hiyo na kuondoka.
Alijiunga na Simba SC kwa mara ya kwanza mwaka 2010 akitokea SC Villa ya kwao. Alicheza Msimbazi hadi mwaka 2013 aliponunuliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola za Kimarekani 300,000 (Sh. Milioni 600 na zaidi).
Hata hivyo, Okwi aliondoka Tunisia baada ya miezi mitatu kufuatia kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo na baadaye kufungua kesi FIFA akiomba aruhusiwe kucheza klabu nyingine kulinda kipaji chake wakati mgogoro wake na Etoile unaendelea.
Etoile ilisitisha huduma kwa Okwi, baada ya kukerwa na desturi ya mchezaji huyo kuchelewa kurejea kujiunga na timu anaporuhusiwa kwenda kujiunga na timu yake ya taifa Uganda.
Akasaini tena SC Villa katikati ya mwaka 2013 kabla ya Desemba mwaka huo, kuhamia Yanga SC- wakati wote huo kesi yake na Etoile ikiendelea FIFA.

Chapisha Maoni

 
Top