0
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Klabu ya Simba Haji Sunday Manara ameishukuru kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini TFF kwa kutengua adhabu yake aliyoipata zaidi ya siku 70 zilizopita.
Manara amesema ni siku muhimu na kubwa Kwa mchezo wa Mpira wa Miguu hususani washabiki wa mchezo huo, baada ya kamati hiyo kuitengua adhabu yake ya kufungiwa mwaka mmoja, kujihusisha na maswala ya kandanda ndani na nje ya nchi.
-Adhabu hii ilikuwa inaiumiza sana, klabu yangu na kuiondolea haki yake muhimu, ya kuwapa habari kwa wakati watanzania juu ya kinachoendelea kwenye Klabu" Alieleza.
Ameendelea kusema kuwa "Kiukweli niishukuru kamati ya nidhamu chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas kwa kuiondoa adhabu hii, kiukweli alioondolewa adhabu sio Haji, ni Simba na mchezo wenyewe wa Soka, Hakika hawa wamesikia kilio cha wengi, na kilio cha wengi kina nguvu ya Mungu Mwenyezi, Shukrani kwa Mola kwa kuwapa nguvu hii kina Tarimba na wenzake" Ameeleza.
Shukrani Kwa Simba.
-Nitakuwa mjinga nisipowashukuru wanasimba wenzangu ambao siku zote wamekuwa upande wangu, hawa ninawaahidi kuwatumikia kwa moyo na dhamira ileile ya Haji ya kuhakikisha haki na wajibu wetu kama klabu unatekelezwa, Kipekee niwashukuru viongozi wangu wa Simba ambao walihakikisha jambo hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka na linamalizika kwa njia ya amani" Alisema.
Manara amesema kuwa hatopenda kufukua makaburi, hivyo yatupasa sote tusonge mbele, na kusema kuwa hakuna aliyeshinda, Bali ulioshinda ni mchezo wa soka.
-Nawaahidi kuendelea kufanya kazi zangu kwa weledi,nidhamu na kwa kuzingatia miiko ya mchezo huu unaobeba dhamana za maisha ya watu walio wengi, sambamba na kuendelea kuitetea na kuilinda klabu yangu kwa nguvu zote" Alimaliza.
Hukumu ya Manara.
Ikumbukwe Aprili 23 mwaka huu, Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilimfungia Haji Manara, kwa mwaka mmoja kutojihusisha na masuala ya soka pamoja na kumpiga faini ya Shilingi Milioni 9.
Manara alikutwa na Makosa Matatu ambayo ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.
Hata hivyo kamati ya nidhamu chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas Leo Jumatatu imetengua adhabu hiyo na kumuachia Huru Haji Manara.

Chapisha Maoni

 
Top