Shujaa wa Taifa Stars leo amekuwa golikipa Said Mohammed Mduda aliyepangua penalti ya Nahodha wa Lesotho
Tanzania imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika michuano ya COSAFA Castle baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanjw wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Shujaa wa Taifa Stars leo amekuwa golikipa Said Mohammed Mduda aliyepangua penalti ya Nahodha wa Lesotho, Thapelo Mokhehle baada
ya Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalaka na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza
ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao,Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua
kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
Ushindi unakuja siku 25 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, mwaka huu katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Romeo Kasengele wa Zambia, aliyesaidiwa na washika vibendera Thomas Kusosa wa Zimbabwe na
Helder de Carvalho wa Angola, ndani ya dakika 90 timu hizo zilishambuliana kwa zamu, Lesotho wakitawala zaidi kipindi cha kwanza na cha pili Taifa Stars wakazinduka.
Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho
wamepata dola 8,300. Fainali ya COSAFA Castle 2017 itachezwa
Jumapili Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe na bingwa atapata dola 42,000 na
mshindi wa pili dola 21,000.
Chapisha Maoni