0
Kikosi cha mabingwa wa Tanzania Bara, Dar Young Africans kimefanya mazoezi ya kwanza asubuhi hii nchini Seychelles kujiandaa na mchezo wa marudiano wa klabu bingwa Africa dhidi ya Saint Louis Suns United.
Yanga ambao walisafiri Jumapili asubuhi wapo nchini humo na kwamba wataendelea na mazoezi mengine jioni ya Jumatatu kuhakikisha wanakuwa fit kabla ya mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa Stade Linité uliopo mjini Victoria, Jumatano ya Februari 21.
Meneja wa timu ya Yanga Hafidh Saleh amesema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na morali waliyonayo ni ya hali ya juu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kusonga mbele.
"Morali ipo juu kabisa, wachezaji wapo salama, wote ni wazima kabisa na wapo tayari kwa mchezo huo wa Jumatano, tumefanya mazoezi asubuhi na jioni pia tutafanya mazoezi mengine," Saleh amesema.
Wachezaji waliopo nchini Shelisheli
Wachezaji ambao wapo na timu nchini Shelisheli ni pamoja na makipa, Ramadhani Kabwili, Beno Kakolanya na Youthe Rostand, wakati mabeki ni Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Gadiel Michael, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Patto Ngonyani na Kelvin Yondani.
Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Raphael Daud, Yussuf Mhilu, Ibrahim Ajib, Said Mussa, Emmanuel Martin, Geoffrey Mwashiuya na Juma Mahadhi,
Mchezo wa awali
Mchezo huo unakuja baada ya mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam, Yanga kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililofungwa na Juma Mahadhi.
Yanga wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya kwanza ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa barani Afrika. Iwapo Yanga watafanikiwa kufudhu katika hatua hiyo watakutana na Mshindi kati ya Township Rollers ya Botswana au El Merreikh ya Sudan.

Chapisha Maoni

 
Top