0
Maandalizi kwa ajili ya kupokea ugeni wa kikao cha Shirikisho la Soka Ulimwengu 'FIFA' utakaofanyika jijini Dar es Salaam Februari 22, yametajwa kukamilika.
Jumla ya mashirikisho 19 ya soka duniani yakiongozwa na Rais wa FIFA Gian Infantino na Ahmad Ahmad wa CAF yanatarajia kushiriki kikao hicho kujadali mada nne muhimu za kukuza soka.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amesema mpaka sasa taratibu zote kwa ajili ya kuupokea ugeni huo zimekwishakamilika na tayari baadhi ya wageni wameanza kuwasili nchini huku wajumbe wengine wakitarajiwa kuwasili mapema siku ya Jumanne.
"Tuna ugeni mkubwa wa FIFA hapa nchini tunategemea kupokea ujumbe wa wageni 70, na tayari ujumbe huo umeshaanza kuwasili nchini kuanzia leo, wameanza kuja wajumbe wa Sekretarieti, lakini Marais wa mashirikisho wenyewe wataanza kuja siku moja kabla ya mkutano wenyewe," Mwakyembe amesema.
Kwa mujibu wa taratibu za mapokezi ya ugeni huo, ni kwamba baada ya Infantino kuwasili nchini ataonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli na kufanya kikao kifupi Ikulu.
Aidha baada ya kikao hicho jioni Rais Infantino na Ahmad Ahmad watazungumza na waandishi wa habari za michezo wa Tanzania ili kuhitimisha kikao hicho cha kihistoria nchini.
Mkutano huu ni sehemu ya mikutano ambayo inafanyika sehemu mbalimbali duniani kwa makundi ya nchi zisizozidi 20 na hivyo muda huu Tanzania ndio imechaguliwa kuwa mwenyeji.
Nchi zitakazoshiriki
Nchi ambazo zitashiriki mkutano huo ni pamoja na Bahrain, Palestina, Saudi Arabia, United Arab Emirates, Algeria, Burundi, Central Africa, Ivory Coast na Mali.
Nyingine ni Morocco, Niger, Tunisia, Bermuda, Monselet, Saint Lucia, US virginal, Congo na Maldives.
Ambapo wajumbe wa mkutano huo ni pamoja na sekretarieti ya uongozi ya CAF, Marais na makatibu wakuu wa mashirikisho 19 ya soka, Rais na baadhi ya wajumbe wa FIFA.
Mada zitakazojadiliwa.
Aidha Mada ambazo zitazungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na Miradi na maendeleo ya Miundombinu ya soka (FIFA Forward Programs), Mada ya pili na Soka la Vijana, Wanawake pamoja na Mashindano ya vilabu(Future of FIFA youths, women and Clubs Competitions).
Mada nyingine itakuwa ni kujadili namna ya kuweza kuboresha Uhamisho wa wachezaji (How to improve the Transfer system and international match Calendar) na mwisho ni vipaumbele vya FIFA ambavyo vitakuwa vimewasilishwa na wajumbe wa mkutano huo.

Chapisha Maoni

 
Top