Mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski amebainisha kuwa anataka alipwe mshahara mkubwa kama anaolipwa mshambuliaji Alexis Sanchez ndani ya Manchester United.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 29 katika Ligi Kuu ya Ujerumani msimu uliopita ameweka wazi kuwa iwapo United au Real Madrid itamuhitaji imtengee mshahara wa Pauni 500,000 kwa wiki.
Lewandowski raia wa Poland amebainisha nia ya kutaka kuondoka Munich lakini Kocha wa timu hiyo amesema hatakubali kumuachia kirahisi.
Mshambuliaji huyo ametaka klabu inayomuhitaji kumtengea fedha za uhamisho za Pauni 70 milioni na mshahara mnono.
Hata hivyo mshahara anaoutaka unaweza kuwa kwakozi kwa United iliapa haitakuja kurudia tena kosa la kumpandishia mchezaji mshahara kwa nia ya kumshawishi ajiunge nayo.
United walimteka Sanchez siku ya mwisho akijiandaa kutua Manchester City, Januari mwaka huu wakamshawishi kwa mshahara mnono wa Pauni 500,000 wiki jambo lililomfanya kuwapuuza City waliokua wakimsubiri akasaini.
Lewandowski amemsihi wakala wake Cezary Kucharski kuhakikisha anaangalia klabu nyingine ikiwa mazungumzo na Rais wa Real Madrid, Florentino Perez hayatazaa matunda.
Madrid ilionyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo kuziba pengo la Cristiano Ronaldo aliyetimkia Juventus huku mshambuliaji mkongwe Karim Benzema akionesha dalili za kutaka kuondoka pia.
Chapisha Maoni