0
MANCHESTER United wamekuwa kwenye hali mbaya baada ya kupoteza mchezo wa pili mfululizo kwenye Ligi Kuu England.
Kocha Jose Mourinho, juzi aliwajibu ovyo waandishi wa habari baada ya timu yake kuchapwa mabao 3-0 na Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Huu ni mchezo wa pili timu hiyo inapoteza baada ya awali kuanguka kwenye mchezo dhidi ya Brighton.

Kocha Muorinho, amesema kuwa hatishwi na matokeo hayo kwa kuwa bado yeye ni kocha bora kwenye Ligi Kuu England na anapendwa sana na mashabiki.
“ Sijali naamini kuwa bado mimi ni kocha bora kwenye Ligi Kuu England na mashabiki wananipenda.
“Mimi ni zaidi ya makocha wengine wote wakikusanya makombe yao hawafikii makombe niliyotwaa ndiyo maana naamini kuwa mimi ni bora kuliko wengine na mnatakiwa kuniheshimu,” alisema Mourinho kwa hasira.
Kocha huyo amesema kuwa pamoja na kupoteza mchezo huo lakini bado anaamini kuwa timu hiyo ni bora na inaweza kufanya vizuri kwenye ligi kwa kuwa ilionyesha kiwango cha juu sana juzi.
“Sijui nini kilikuwa kibaya kwetu, tulicheza vizuri lakini mwisho tukapoteza mchezo, tuliingia mapumziko tukiwa na nguvu, lakini ghafla mambo yakabadilika kipindi cha pili.
“Ukiruhusu mabao mawili ya haraka, ni rahisi kushindwa kuhimili, lakini naamini kuwa tunaweza kuamka tena na kufanya vizuri kwenye ligi msimu huu,” alisema Mourinho.

Chapisha Maoni

 
Top