Timu ya Taifa Tanzania chini ya miaka 17 'Serengeti Boys', Leo hii imeonyesha kandanda safi kabisa dhidi ya timu ya vijana Rwanda baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0.
Katika mchezo huo Serengeti walikuwa wakicheza kwa kutulia sana na kupiga pasi za kuonana, huku katika safu ya kiungo ikiongozwa na nahodha wake Morice Abraham.
Rwanda wanaonolewa na Rwasamanzi Yves, nao walionekana kukomaa katika kutengeneza nafasi na kucheza mpira lakini wachezaji wake walikuwa kama wamekosa utimamu wa mwili (Fitness) na kupokonywa mipira kwa urahisi.
Dakika 23 Serengeti walipata bao kupitia kwa Kelvin John, ambaye aliingia na mpira mpaka ndani ya dimba na kisha aliwachambua mabeki mpaka kipa Pierre Ishimwe na kuweka kimiani.
Baada ya kupata goli hilo, Serengeti walianza kucheza mpira wa jukwaani (Show Game), hali iliyofanya mashabiki waliojitokeza uwanjani kubaki midomo wazi.
Serengeti waliweza kuwazuia Rwanda kutoingia katika kumi na nane yao, zaidi ya dakika 10 (24 mpaka 35) na kuwafanya Rwanda wacheze nusu uwanja.
Kipindi cha pili Serengeti walianza kwa kufanya shambulio la hars katika dakika 45, ambapo Kelvin john alipiga shuti lakini liliokolewa na Eni aniyomugusha na kuwa kona isiyokuwa na faida.
Rwanda walionekana kuanza kusaka bao la kusawazisha kwa kutumia mbinu ya kupiga nje ya kumi na nane, ambapo dakika 55 Kelvin Ndori alipiga shuti kali lakini liliishia usoni kwa mchezaji mwenzake Aime Nshuti.
Dakika 70 Rwanda walifanya shambulizi la hatari kupitia kwa mshambuliaji wao Kelvin Ndori lakini kipa wa Serengeti, Shaban Hassan aliucheza na kuwa kona isiyokuwa na faida.
Dakika 73 mchezaji aeric Niyonsenga aliadhibiwa kwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi kwa kumkwatua kwa nyuma mshambuliaji wa Serengeti Kelvin John.
Dakika 78 Serengeti Boys walipata bao kupitia kwa Agiri Ngoda baada ya kufanyika uzembe kwa kipa wa Rwanda, Pierre Ishimwe aliyepiga shuti na kumgonga Kelvin John na mchezaji huyo alimchambua na kupiga pasi ya mwishonkwa Ngoda na kuiandikia Serengeti bao la pili.
Serengeti walionekana kutotosheka na mabao kwani walikuwa wakitengeneza nafasi na dakika 83, kiungo Pascal Msindo alipopiga pasi iliyopita katikati ya mabekibwa Rwanda, lakini spidi ya Kelvin John ilisaidia kuwapita na kuweka mpira wavuni kwa ustadi mkubwa.
Dakika 90 Kelvin John alifunga bao la kufuta kabisa matumaini kwa Rwanda.
Serengeti wanaongoza kundi A kwa pointi 9, huku Rwanda wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 6 katika michezo mitatu na nafasi ya tatu ikishikiliwa na Burundi huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Sudan
Chapisha Maoni