Pamoja na kupewa nafasi kubwa kuibuka na ushindi mnono kwenye mechi yake dhidi ya Tanzania Prisons, Simba ililazimika kufanya kazi ya ziada ili kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao la mapema lililopachikwa dakika ya pili na mshambuliaji Meddie Kagere lilitosha kuipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande hao wa Tanzania Prisons.
Hata hivyo, licha ya kupachika bao hilo la mapema Simba walijikuta wakihaha kulilinda kutokana na kiwango bora kilichoonyeshwa na wapinzani wao hasa kipindi cha pili.
Simba iliyoanza kutawala mchezo kipindi cha kwanza ilionekana kukosa ubunifu wa kupenya safu imara ya ulinzi ya Prisons ambayo ilicheza kwa nidhamu na umakini wa hali ya juu huku ikitibua mashambulizi na mipango yote ya Simba.
Bao hilo la Kagere lilidumu hadi mapumziko, lakini timu hizo ziliporudi kipindi cha pili, Prisons ilibadilika na kutawala mchezo huku ikipeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Simba.
Uimara wa safu ya kiungo ya Prisons iliyoundwa na Jumanne Elfadhil sambamba na Cleophace Mukandala ilionekana kuwa kikwazo kwa Simba, ambayo ilijikuta ikichoka na kushindwa kuhimili mikiki.
Hata hivyo, pamoja na Tanzania Prisons kumiliki mpira na kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Simba, ilishindwa kuzitumia nafasi hizo kupata bao la kusawazisha.
Kocha wa Tanzania Prisons, Mohammed Abdallah 'Bares' alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Salum Bosco na Ismail Aziz na nafasi zao zilichukuliwa na Hassan Kapalata na Ramadhan Ibada.
Kwa upande wa Simba iliwatoa John Bocco, Shiza Kichuya na Hassan Dilunga na kuwaingiza Mzamiru Yassin, Adam Salamba na Nicholas Gyan.
Mabadiliko hayo hayakuwa na maajabu kwa timu zote kwani, hayakubadili matokeo ya mchezo hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa
Chapisha Maoni