Tottenham waliendeleza mwanzo wao mwema wa Ligi Kuu England msimu huu kwa kuwafunga Manchester United mabao matatu bila jibu na kumuongezea shinikizo meneja wa United Jose Mourinho.
Mechi hiyo ilichezewa Old Trafford.
Mourinho alikuwa anatumai kwamba mashetani hao wekundu wangejikwamua kutoka kwa uchezaji mbaya uliochangia kuchapwa kwao ugenini na Brighton.
Lakini Spurs walionesha kwamba hawakuwa tayari kuwaruhusu United kutawala na Harry Kane na Lucas Moura waliwapangua na kuwafunga mabao mawili katika kipindi cha dakika mbili mapema kipindi cha pili.
United walisalia majuto tu baada ya Romelu Lukaku kupoteza nafasi ya wazi hata baada ya kumchenga kipa Hugo Lloris baada ya kupokea pasi kutoka kwa Danny Rose.
Mwisho msiba ukawa umefika na United wakawa wameandikisha mwanzo mbaya zaidi wa msimu tangu msimu wa 1992-93.
Kane alitangulia kufunga dakika ya 50 kwa kichwa na kuwazawadi Spurs bao lao la kwanza na Moura akafuatiliza kwa bao jingine muda mfupi baadaye kutokana na pasi ya Christian Eriksen.
Moura alichomoka na kuongeza la tatu dakika sita kabla ya mechi kumalizika na kukamilisha ushindi wa Spurs.
Mourinho alionekana kutamaushwa na matokeo hayo na hali kwamba mashabiki wengi waliondoka uwanjani kabla ya mechi kumalizika.
Sasa ameshindwa mechi mbili kati ya tatu za mwanzo wa msimu kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yake ya ukufunzi.
Mwenzake Mauricio Pochettino, ni kinyume, kwani ameonja ushindi wake wa kwanza kama meneja wa Spurs uwanjani Old Trafford, mechi nne za karibuni zaidi wakiwa walikuwa wamechapwa bila kufunga bao hata moja la kufutia machozi.
Kabla ya ushindi huo, Spurs walikuwa wameshinda mechi moja pekee kati ya 12 dhidi ya 'klabu sita kubwa' Ligi ya Premia, tangu walipowalaza Manchester City Februari 2016, kwa hivyo matokeo haya ya Jumatatu yatawatia moyo sana katika juhudi zao za kutaka kushinda Kombe.
Mchezaji bora wa mechi - Lucas Moura (Tottenham)
Mourinho: 'Siuchukulii huu kuwa wakati mgumu'
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho
aliambia BBC Sport baada ya mechi: "Mashabiki ndio waamuzi bora zaidi kwenye mechi na walifanya vyema sana kwa wachezaji.
"Nilitaka kuhakikisha kwamba mashabiki walipata wanachostahili kutoka kwetu na nilitaka kutenda haki kwao kwani wamekuwa wazuri sana. Siuchukulii muda huu kuwa wakati mgumu.
"[Sisi tulikuwa] ndiyo timu bora, timu iliyoshambulia, timu iliyoshambulia sana, iliyounda nafasi nyingi na iliyopoteza nafasi nyingi, lakini kisha kuanzia kwa kona ya kwanza waliyoipata Tottenham walifunga bao moja na kuanzia hapo wakawa ndiyo timu iliyoumudu mchezo."
"Nimesikitika lakini nawafurahia wachezaji na uchezaji wao. Tuliunda nafasi nyingi leo kuliko kwenye mechi nyingi zetu za awali.
"Nilichokuwa najaribu kufanya ni kuwapa motisha na hilo si jambo rahisi. Kawaida, unapocheza vyema huwa unashinda, na hilo ndilo huwa sitaki kuruhusu lipotee kwenye mechi. Bao moja linafungwa na mambo yote yanaweza kubadilishwa na hilo."
Kuhusu mabeki wa Manchester United, alisema: "Tulifanya vyema sana wiki yote lakini kuna mambo ambayo huwezi kuyatatua."
Meneja wa Tottenham Mauricio Pochettino
aliambia BBC Sport: " Ni ushindi mkubwa sana kwetu na najionea fahari sana kutokana na uchezaji wetu.
"Huwa vigumu sana kuwachapa Manchester United uwanjani Old Trafford. Walikuwa ndio wanaoongoza kwa mchezo kipindi cha kwanza lakini tulitawala baada ya hapo, na hali kwamba hatukufungwa ni bonasi.
"Ni mwanzo tu wa msimu na tunahitajika kuendeleza haya. Tunahitai kuukubali uhalisia lakini tuendelea kujituma na kujiboresha. Wengi wa wachezaji wetu wamefanya mazoezi kwa wiki tatu pekee, lakini tunataka kujenga kitu cha kipekee."
Nini kinafuata?
United watasafiri Turf Moor kucheza na Burnley nao Tottenham wakutane na Watford uwanjani Vicarage Road, mechi zote mbili zikichezwa Jumapili 2 Septemba kuanzia saa kumi na mbili jioni saa za Afrika Mashariki.
Chapisha Maoni