0
Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku
maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), yaliyotarajiwa kuanza kufanyika leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Jeshi hilo limeonya kuwa maandamano hayo ni batili na ni kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana makao makuu ya jeshi la Polisi Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja alisema jeshi hilo limeanza kupokea
taarifa ya chama hicho, kikitaka kufanya
maandamano kuanzia leo. Lakini, alisisitiza kuwa maandamano hayo hayataruhusiwa.

“Septemba 15 jeshi lilitoa taarifa kuhusu kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwahimiza wafuasi wa chama chake
kufanya maandamano na migomo isiyokoma pote nchini ili kusitishwa kwa Bunge la Katiba na hivi
sasa tumeanza kupokea taarifa ya chama hicho kufanya maandamano,” alisema.

Alisema maandamano hayo ni batili, kwa sababu Bunge la Katiba linaloendelea hivi sasa, linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hakuna sheria iliyokiukwa, hivyo
kitendo cha kufanya maandamano, kushinikiza kuvunjwa kwa Bunge hilo ni kinyume cha sheria,
jambo ambalo jeshi la polisi haliwezi kuruhusu.

Aidha, alisema kuwa ieleweke wazi kwamba Bunge la Katiba, lipo kisheria na kila jambo linalofanyika bungeni ni kwa mujibu wa sheria. Chagonja alisema jeshi la polisi lina jukumu la
kulinda watu wote, wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

“Hata hivyo, hivi sasa kuna kesi inayoendelea Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayohoji uhalali wa kuendelea kwa Bunge hilo na kesi hiyo
haijafikia mwisho na uamuzi kutolewa, hivyo maandamano hayo yaliyopangwa na Chadema yanaingilia uhuru wa Mahakama, jambo ambalo
siyo sahihi. Mahakama kama chombo cha kutoa haki, kiachwe kifanye kazi yake,” alisema.

Chagonja alitoa mwito kwa wananchi wote, kuendelea na shughuli zao na yeyote atakayekiuka katazo hilo, jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Wakati Chagonja akiyasema hayo, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, amewaonya wafuasi wa Chadema wanaodaiwa kutaka kuandamana hadi
Viwanja vya Bunge kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la
Katiba.

Hata hivyo, uongozi wa Chadema mkoani humo, umedaiwa kusisitiza maandamano yako palepale.
Akizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula alisema maandamano hayo, pia yamepangwa kufanyika
katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma.
Alisema juzi walipokea taarifa kutoka kwa Uongozi wa Chadema Mkoa wa Dodoma, juu ya kufanya
maandamano ya amani kuanzia viwanja vya Nyerere Square hadi viwanja vya Bunge kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana.

Alisema taarifa ya maandamano kama hayo, yanayotarajia kufanyika katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma, ilitolewa jana ambapo ni muda
ulio kinyume na sheria ya kutoa taarifa za maandamano ndani ya saa 48.

Alisema katika barua ya chama hicho kwenda kwa Jeshi la Polisi, viongozi wa Chadema wa Mkoa huo, walisema wanapinga Bunge la Katiba na
wanataka kupaza sauti zao, zisikike dunia nzima na walisisitiza kufanya maandamano hayo leo. “Walikuja hapa viongozi wa Chadema Mkoa,
tulikaa nao kwenye mazungumzo zaidi ya saa mbili, tuliwaambia Bunge lipo kwa mujibu wa sheria za nchi na hakuna mahakama iliyotamka Bunge lisitishwe, lakini walisisitiza kuwa maandamano yako pale pale,” alisema.

“Maandamano hayo ni batili yanapinga chombo ambacho kipo kwa mujibu wa sheria, tunasisitiza wananchi wa Dodoma wasishiriki maandamano
hayo, hayana tija hata kidogo na wananchi wasijitokeze waendelee na shughuli zao,” alisema.

Alisema maandamano ni haki ya kikatiba, lakini wanatakiwa kufuata sheria. Alisema Jeshi la Polisi
limejipanga kudhibiti maandamano hayo katika wilaya zote, kutokana na viongozi wa Chadema kukaidi amri ya kutaka kusitisha maandamano hayo.

Wakati jeshi la Polisi likichukua hatua hiyo, Umoja wa Vijana Wazalendo wa Vyuo vya Elimu ya Juu Dar es Salaam, nao umejitokeza na kulaani kauli
zilizotolewa na Mbowe za kuhamasisha
maandamano na migomo nchi nzima, hata kama jeshi la Polisi halitabariki kufanyika kwa mambo
hayo.

Mwenyekiti wa Umoja huo, Mussa Omar
anayesoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), alisema umoja huo ni Muungano wa vyuo 14 vya
elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam.
Alisema Watanzania wengi wamekerwa na kusononeshwa na kauli ya kiongozi huyo ya kuhamasisha maandamano, alizozitoa wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa
Chadema, mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

“Tumemsikia akiahidi maandamano bila kikomo kwa kibali cha polisi au bila kibali cha polisi mbele ya wajumbe na wageni ambao wengine sio
Watanzania,” alisema Omar.
Aliongeza kuwa kauli kama hiyo, haiwezi
kusemwa hata na Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.

Alimtaka Mbowe afahamu dhamana kubwa ya uongozi aliyonayo kwa wafuasi wake na Watanzania kwa ujumla, wakimtaka afuate misingi
ya sheria za nchi, katiba na utawala bora.
Pia, alisema kauli zilizotolewa na Mbowe, hazibebeki na mtu yeyote katika taifa hili, kwani alitoa kauli mbaya kuliko zote kisiasa, ambazo
zimewahi kusemwa majukwaani.

“Watanzania tukikaa bila kuzilaani na kuzikemea kauli zake tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe
na pia hatuvitendei haki vizazi vijzvyo vya nchi yetu,” aliongeza.
Alihoji uhalali wa kutoa amri hizo kwa wafuasi wake, ilhali ni kiongozi tu wa chama, tena ambacho hakiko madarakani.

Alisema Watanzania wanapaswa kuwakataa viongozi wenye jazba na kutumia mabavu katika
kutimiza majukumu yao, kwani wanaweza kuiingiza nchi katika vurugu zisizo na ulazima. Pia alivitaka vyombo vya dola, visizivumilie kauli
kama hizo, zilizotolewa na Mbowe, kwani vyombo vya dola vina dhamana ya kulinda, kutunza na
kuendeleza amani na utulivu wa nchini, wachukue hatua kali za kisheria kwa kauli ya kutishia uvunjifu wa amani kabla hajaingiza nchi kwenye
machafuko ya kisiasa.

Wakati huo huo, viongozi wa juu wa chama hicho, leo wamepanga kumsindikiza Mbowe kwenda
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini, ambako ameitwa kwa barua.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema Mbowe alipokea barua, ikimtaka afike Makako Makuu ya jeshi hilo leo saa 5:00 asubuhi.
“Mwenyekiti wetu ameitwa Makao Makuu ya Polisi leo na hatujui kaitiwa nini, huenda anakwenda
kuhojiwa na huenda mwito huo umetokana na kauli alizotoa awali katika mkutano mkuu, ambazo zililenga kuhamasisha maandamano ya
nchi nzima kupinga Bunge la Katiba
linaloendelea”, alisema Dk Slaa.
Alitaja watakaoongoza msafara wa amani wa kumsindikiza Mbowe kuwa ni mwanasheria wao, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu,
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Profesa Abdallah Safari na Mwanasheria Peter
Kibatala.

Hata hivyo, alisema pamoja na kiongozi huyo kuitwa na polisi, bado jeshi hilo haliwezi kuvunja ajenda ya kuandamana, kwa kuwa ilipitishwa na
Kamati Kuu ya chama hicho, na kwamba polisi wao wanapaswa kutoa kibali cha kuruhusu maandamano hayo.

Awali, alisema maazimio yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho ni kuunganisha nguvu ya pamoja na vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) .
Alisema maazimio hayo, yataanza Desemba 14, mwaka huu, siku ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa unaanza.

Alieleza kwamba chama hicho kimeunda kamati ya watu watano, itakayoangalia jinsi ushirikiano wa Ukawa utakavyokuwa kwenye uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutoka kwao nje bungeni, kulikuwa sahihi. Alisema katiba mpya, haiwezi kupatikana leo au kesho.

Chapisha Maoni

 
Top