Wanamgambo 17 wa Al-Shabaab wakamatwa mkoani Arusha.....Wanatuhumiwa kulipua bomu Arusha Night Park, wawili wasomewa kesi hospitalini
Polisi imesema imekamata watu 17,
wanaotuhumiwa kuhusika na ulipuaji wa
mabomu jijini Arusha na usajili wa vijana kwa
lengo la kuwasafirisha kwenda nje ya nchi,
kujiunga na vikundi vya kigaidi ikiwemo Al
shabab.
Pia, watu hao wanatuhumiwa kutaka kulipua
maeneo mengine, hasa taasisi za Serikali na
maeneo ya mikusanyiko ya watu.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini
(DCI), Isaya Mungula alitoa taarifa hiyo jana
kwa waandishi wa habari jijini Arusha, muda
mfupi kabla ya watuhumiwa kufikishwa na
kusomewa mashitaka hayo mahakamani.
Mungula alisema kukamatwa kwa watu hao,
kunatokana na tukio la Aprili 13 mwaka huu
saa 1.30 usiku katika baa ya Arusha Night
Park . Katika mlipuko huo, unaosadikiwa kuwa ni wa
bomu, watu 14 walijeruhiwa na mmoja, Sudi
Ramadhani, alifariki mwezi mmoja baada ya
tukio hilo.
DCI Mungula alisema siku hiyo ya Aprili 13
mwaka huu saa 4.28 usiku, bomu lingine
lililotengenezwa kienyeji, lilibainika kutegwa
katika baa ya Washington, lakini liliondolewa
eneo hilo bila kuleta madhara.
Kwa mujibu wa Mungula, baada ya matukio
hayo, upelelezi ulianza mara moja. Kwa
kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama,
sanjari na kupata maelezo ya mashuhuda wa
tukio na katika upelelezi, ilibainika bomu la
Arusha Night Park na baa ya Washington,
yanafanana na yametengenezwa kienyeji. Kwa upande wa mabomu yaliyotokea katika
Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi
Parokia ya Olasiti jijini Arusha na katika
mkutano wa kampeni wa Chadema eneo la
Soweto, ni mabomu yaliyotengenezwa
kiwandani.
Alisema watuhumiwa hao, pia imebainika
wanahusika kufanya mikakati ya mashambulizi
katika maeneo mengine na sehemu mbalimbali
nchini, ambazo ni taasisi za Serikali na sehemu
za mikusanyiko ya watu.
Alitaja waliokamatwa, wakituhumiwa kuhusika
na matukio hayo ya ulipuaji mabomu ni
Abdallah Labia (34), maarufu kwa jina la Bro
Mohamedi , mkazi wa Mang’ola wilayani
Karatu Mkoa wa Arusha.
Wengine ni Abdulkarim Hasia (32) mkazi wa
Nguselo jijini Arusha, Hassani Said (23) mkazi
wa Tengeru wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Pia, wamo wakazi watatu wa Magugu wilayani
Babati mkoani Manyara, ambao ni Rajabu
Hemedi (28), Ally Kidaanya (32) na Shabani
Wawa (22). Watuhumiwa wengine ni Abdallah Wambura
(40) mkazi wa Mromboo –Murriet jijini
Arusha, Ally Jumanne (25) mkazi wa Matufa
Babati mkoani Manyara na Yassini Sanga (26)
mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga.
Watu nane wanaotuhumiwa kukusanya vijana
na kuwasafirisha kwenda nje ya nchi, kujiunga
na vikundi vya kihalifu ni Swalehe Hamisi (51)
mkazi wa Sombetini jijini Arusha, Abdallah
Yassini (33) mkazi wa Tunduru, Sudi Nasibu
Lusuma (18) mkazi wa mkoani Mwanza na
Abdallah Nyakwela (46), mkazi wa Sakina, jijini
Arusha.
Watuhumiwa wengine ni Maka Gewa (19)
mkazi wa Bunda mkoani Mara, Abdulrazak
Mohamed (25) wa Tunduru, Abdallah Labia
‘Bro Mohamedi’ na Hassani Said (23) mkazi wa
Tengeru wilayani Arumeru, Arusha. Mungula alisema Polisi inaendelea kusaka
watu wengine 25, wanaotiliwa shaka kuhusika
katika matukio ya mwaka jana ya milipuko ya
mabomu ya Olasiti na Soweto.
Alitaka wananchi kuendelea kutoa taarifa na
ushirikiano kwa jeshi hilo, kufichua wahalifu
wa ndani na nje wa matukio hayo.
Watuhumiwa 15 wa mlipuko wa bomu katika
baa ya Arusha Night Park waliofikishwa
mahakamani jana, walisomewa mashitaka 16.
Miongoni mwa mashitaka waliyosomewa ni
kuua, kukusudia kuua, kusafirisha binadamu
na kusajili vijana kujiunga na kikundi cha
kigaidi cha Al-Shabaab.
Waendesha mashitaka wa Serikali, Khalili
Muda na Marcelino Mwamunyange, walidai
watuhumiwa waliua na kukusudia kuua Aprili
13 mwaka huu saa 1.30 usiku katika baa ya
Arusha Night Park .
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Mkoa wa Arusha, Mustapha Siani, ilidaiwa
washitakiwa waliua mtu mmoja na kujeruhi
watu 14. Mwendesha Mashitaka, Muna alisoma
mashitaka kwa washitakiwa 13, kati ya 15,
waliokuwa kizimbani. Washitakiwa wawili
hawakusomewa mashitaka, kwani walikuwa
wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Arusha ya Mount Meru, wakipata matibabu.
Vile vile Mahakama ilihamia katika hospitali
hiyo, kusomea washitakiwa hao wawili
mashitaka ya kuua, kukusudia kuua,
kusafirisha binadamu na kusajili vijana
kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab
Waliolazwa hospitalini hapo ni Abdulkarimu
Hasia (32), mkazi wa Ngusero jijini Arusha na
Rajabu Hemed (28), mkazi wa Magugu wilayani
Babati.
Walioshitakiwa kusafirisha vijana na kujiunga
na kikundi cha kigaidi ni Athumani Labia (34),
Ally Kidaanya(32), Abdallah Thabit (32) na
Abdallah Wambura (40) . Wengine ni Hassani
Saidi (23), Ally Jumanne (25), Yassini Sanga
(26) na Shabani Wawa(22).
Washitakiwa sita waliosomewa mashitaka ya
kuua na kukusudia kuua ni Swalehe Hamisi
(51), Abdallah Yasini (33), Sudi Lusumu (18),
Abdallah Nyakwela (46), Maka Gewe (19) na
Abdulrazak Mohamed (25).
Wote hawakutakiwa kujibu chochote, kwani
mahakama hiyo kisheria haiwezi kusikiliza kesi
hiyo, ambayo itatajwa tena Juni 11 na 12
mwaka huu.
Chapisha Maoni