0
Wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba jana walianza kupiga kura za kuamua ibara za Katiba inayopendekezwa, huku kura za wajumbe kutoka Zanzibar zikiibua wasiwasi wa iwapo theluthi mbili
itapatikana au la.

Dalili za kupiga kura za hapana kutoka upande wa Zanzibar zilianza kujionyesha mapema baada ya
taarifa za ndani kueleza kuwa zikikosekana 10 kutoka upande huo wa Muungano hakuna katiba.

Hata hivyo, mapema Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alisema idadi ya kura zinazohitajika kukidhi theluthi mbili kwa upande wa Zanzibar ni
140 na jana jioni waliokuwamo bungeni walikuwa 142.

Mjumbe wa kwanza kufungua pazia kwa kura ya hapana alikuwa ni Adil Mohamed Adil aliyepiga
ibara zote 157 kwa sura ya kwanza hadi 10. Wengine waliopiga kura ya hapana kwa sura zote ni Dk Alley Soud Nasoro na Salma Said.

Waliopiga kura za hapana ni Fatuma Mohamed Hassan na Jamila Abeid Saleh, huku baadhi ya wajumbe wakipiga kura za siri.
Kwa upande wake, Ali Omary Juma, alikubaliana na sura za 2, 4, 5 na 9 lakini akizikataa sura za 1,3,6,7,8 na 10.

Kwa upande wa Tanzania Bara, wajumbe Abia Nyabakari na Dk Ave-Maria Semakafu walipiga kura za ndiyo kwa baadhi ya sura na zingine
kuzikataa.

Mjumbe Ali Keissy Mohamed aliushangaza ukumbi kwa kupiga kura ya ndiyo kwa sura zote tofauti na wakati akiwa katika vikao vya kamati
ambapo alikataa muundo wa serikali mbili.
Watakaopiga kura kwa faksi
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana alitangaza orodha ya wajumbe 22 wanaotarajiwa kupiga kura kwa njia ya faksi au
mtandao wakiwa nje ya Bunge hilo.
Katika orodha hiyo, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, wajumbe
tisa wako Saudi Arabia kwa ajili ya Hijja, wawili India kwa matibabu, mmoja yuko masomoni Uholanzi na wengine nje ya Dodoma lakini yuko hapa nchini.

Orodha ya wajumbe
Wajumbe walioko Uarabuni ni Dk Abdalah Kigoda, Mussa Yusuph Kundecha, Hamza Mustapha Njozi,
Mohamed Raza, Dk Maua Daftari, Shawana Bukheri Salum, Asha Dodo Mtwangi, Amina Andrew Clement na Riziki Lulida.
Wajumbe walioko India kwa matibabu ni Beatrice Shelukindo na Salum Hassan Turk. Wajumbe wengine waliko nje ya nchi ni Fredrick Msigala, Waziri wa Afya, Dk Seif Suleiman Rashid,
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela. Waliopo nchini ni Esther Bulaya, William Lukuvi,
Profesa Esther Mwaikambo, Dk Athman
Mfutakamba, Saada Salum Mkuya, Dk Henry Nyamubi, Sixtus Mapunda na Dk Natujwa Mvungi.


Credit: Mwananchi

Chapisha Maoni

 
Top