0
Watu sita wakiwamo wahudumu watatu
wa afya wa hospitali teule ya Wilaya ya
Sengerema mkoani Mwanza,
wamewekwa chini ya uangalizi maalum
baada ya kumhudumia mgonjwa
aliyefariki akiwa na dalili za ugonjwa wa
ebola.Mtu aliyefariki alitajwa kuwa ni
Salome Richard (17), anayetoka katika
kijiji cha Kahunda wilayani
Sengerema.Akithibitisha kuwapo kwa
hali hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali
Teule ya Wilaya ya Sengerema, Dk. Mary
Jose, alisema mgonjwa huyo alifikishwa
katika hospitali hiyo na ndugu zake
watatu akiwa na homa kali huku
akitokwa na damu sehemu mbalimbali
za mwili wake.Alisema vipimo vya
mgonjwa huyo vimepelekwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
“Tulimpokea juzi saa 7 mchana kutoka
katika kijiji cha Kahunda wilayani hapa
akiwa na homa kali akitokwa damu
mwilini, lakini kwa tahadhari tulimweka
wodi maalum peke yake akipatiwa
matibabu na ilipotimu saa 8 usiku
alifariki dunia,” alisema
Alisema kutokana na tahadhari ya
ugonjwa huo, watumishi watatu wa idara
ya afya na ndugu watatu wa marehemu
huyo, wamezuiliwa kwa kuwekwa katika
uangalizi maalum hadi matokeo ya
vipimo vilivyochukuliwa
vitakaporejeshwa toka Muhimbili.
Akizungumzia tukio hilo, muuguzi
Mfawidhi wa hospitali hiyo, Daniel
Mihayo, alisema timu maalum ya
watalaam na viongozi wa mkoa walienda
hospitalini hapo juzi na kuondoka na
vipimo vya mgonjwa huyo kabla
hajafariki dunia kwa kuzingatia
maelekezo ya serikali ya kuchukua
tahadhari linapotokea tukio kama hilo.
“Kwa sasa jamii inatakiwa kuepukana na
uzushi uliozagaa kila kona kuhusu
mgonjwa huyo kufariki kwa ebola…
tunawamba wasiwe na wasiwasi kwani
hatua stahiki zinachukuliwa kwa
wagonjwa wa aina hiyo kama tahadhari,”
alisema Mihayo.
Mhudumu aliyempokea mgonjwa huyo
katika hospitali hiyo, Fungameza Majula,
alisema ndugu watatu walimpeleka
mgonjwa huyo kwa taksi lakini
alipobaini dalili hizo aliujulisha uongozi
wa hospitali na mara moja hatua za
tahadhari zilichukuliwa ikiwa ni pamoja
na kuwazuia ndugu kurudi nyumbani.
Hata hivyo, juhudi za kumpata mkuu wa
Wilaya ya Sengerema, Careen Yunusu,
kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa.
Akizungumzia tukio hilo, Mganga mkuu
wa mkoa wa Mwanza, Bw.Valentino
Bangi, alisema alipokea taarifa za
mgonjwa huyo kufariki kwa homa
inayofanana na ugonjwa wa ebola au
maburgh.
Bw.Bangi alisema ofisi yake imetuma
timu ya wataalam wa afya katika
Hospitali ya Wilaya Sengerema na
kuchukua sampuli ya vipimo vya
mgonjwa na kupeleka Muhimbili kwa
uchunguzi zaidi.
Bw.Bangi alisema ili kukabiliana na
mlipuko wa magonjwa hayo, tayari taifa,
uongozi wa mkoa wa Mwanza kwa
kushirikiana na ofisi yake, wameweka
vituo vya kupima magonjwa katika
mipaka ya Sirari, Mutukula na uwanja
wa Ndege wa Mwanza.

Chapisha Maoni

 
Top