MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,jijini Dar es Salaam, jana iliamuru mashindano ya urembo Tanzania yaliyopangwa kufanyika Oktoba 11, mwaka huu kuendelea
baada ya kutupilia mbali maombi ya
dharura yaliyowasilishwa na Prashant
Patel dhidi ya Hashimu Lundenga ya kuzuia kuendelea kuendesha kinyang'anyiro hicho
kwa madai ya kukiuka mkataba wa
makubaliano yao.
Kadhalika mahakama hiyo imesema
maombi ya hati ya dharura
yaliyowasilishwa na Patel hayana mashiko
ya kisheria na kwamba kuzuia kufanyika
mashindano hayo ambayo wadhamini
mbalimbali wamewekeza fedha zao
itasababisha mgangano wa kimaslahi.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu
Mkazi Frank Moshi baada ya kusikiliza
hoja za mawakili wa pande zote mbili
kuhusu maombi hayo ya dharura ya kuzuiabmashindano hayo kufanyika Oktoba 11,
mwaka huu.
Hakimu Moshi alisema mlalamikaji
amefungua kesi mahakamani hapo pamoja
na maombi ya hati ya dharura akiitaka
mahakama yake kuzuia mashindano
kufanyika kutokana na mlalamikiwa
kuvunja haki dhidi ya mwanzilishi
mwenzake Patel.
Alisema Patel kupitia hoja za maombi yake, amedai kuwa Lundenga alivunja mkataba
huo kwa kufanya mawasiliano moja kwa
moja na mawakala bila kumshirikisha.
Hata hivyo, mahakama bila kuacha shaka
imeona hakuna sababu za msingi katika
hati hiyo ya kusababisha mashindano hayo
yasifanyike na kwamba hayawezi kuathiri kesi ya msingi iliyofunguliwa na
mlalamikaji huyo.
“Mahakama imeona hakuna sababu ya
kuzuia mashindano hayo kwa sababu
wadhamini na washiriki wametumia
gharama zao na kwamba kwa kufanya
hivyo kutasababisha mgongano wa
kimaslahi” alisema Hakimu Moshi wakati
akitupilia mbali hati hiyo ya dharula.
Akifafanua zaidi alisema hati ya dharura
ya mlalamikaji haina mashiko kisheria kwa sababu kesi yake ya msingi ipo
mahakamani na kwamba haina uhusiano na mashindano yatakayofanyika Oktoba 11,
mwaka huu.
Mapema juzi, mahakama hiyo ilitupilia
mbali pingamizi la awali la Lundenga
lililotaka hati hiyo ya dharura kutupilia
mbali.
Chapisha Maoni