MWANAMKE Sakina Kopa (41) amefariki dunia siku tatu baada ya kupigwa na kujeruhiwa na mumewe anayedaiwa kuchukizwa kwa kumkuta akiwa baa usiku.
Aidha, katika tukio jingine linalohusishwa na wivu, dereva wa bodaboda amemjeruhi kwa visu mpenzi
wake ambaye ni Mwalimu, na baada ya kudhani amemuua, naye alijichoma kisu hadi utumbo kutoka nje, ingawa bado yu hai.
Matukio hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paul. Tukio la kwanza lilitokea Oktoba 22, mwaka huu saa 4
usiku katika maeneo ya baa ya Mafiga, Manispaa ya Morogoro, likimhusisha Sakina na mumewe.
Kamanda Paul alisema mwanamke huyo alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Mkoa akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa kufuatia kipigo kutoka kwa mumewe, Hamisi Yohana baada ya
kukutwa akiwa katika baa hiyo.
Alisema baada ya mwanamume huyo kumkuta mkewe akiwa baa, alimpiga na kumjeruhi vibaya katika maeneo mbalimbali ya mwili wake ikiwemo
tumboni na usoni, hali iliyosababisha akimbizwe hospitalini.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Oktoba 25, mwaka huu mwanamke huyo alifariki dunia akiwa hospitali na mtuhumiwa amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamni mara uchunguzi utakapokamilika.
Katika tukio la pili lililotokea Oktoba 27, mwaka huu saa 1:30 asubuhi katika Mtaa wa Mkwajuni, Kamanda Paul alisema linamhusisha mwendesha
bodaboda, Raphael Bernard (33) mkazi wa Kichangani na Rosemary Mkoba (33), Mwalimu wa Shule ya Msingi Mafisa, mjini Morogoro.
Alisema siku ya tukio, Bernard alikwenda
nyumbani kwa mpenzi wake Rosemary kumhoji sababu za kutokuwa mwaminifu kwenye mahusiano yao, hali iliyozusha ugomvi baina yao
na hivyo kuanza kumchoma kisu mwalimu huyo
katika maeneo mbalimbali ya mwili ikiwa ni pamoja na mikononi, tumboni na kichwani. Aliongeza kuwa, kutokana na kelele za kuomba msaada za mwalimu huyo, watu walianza kukusanyika kwa lengo la kutoa msaada na Bernard alipoona mwenzake anazidiwa, aliamini
amemuua hivyo alichukua uamuzi wa kujifungia ndani na kujichoma kisu tumboni hali iliyosababisha utumbo kutoka nje.
Alisema majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wakipatiwa matibabu na kwamba hali zao si nzuri.
Chapisha Maoni