KAMATI ya Bunge inayoshughulikia Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeishauri Serikali kuifuta Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya kubaini
upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 40.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajab Mohammed Mbarouk alishauri hayo jana wakati wa kikao cha kupitia taarifa ya CAG ambapo alisema ubadhirifu
huo ni wa kati ya mwaka 2010 hadi 2013.
Alisema hesabu za miaka hiyo ndizo zenye matatizo ambapo watendaji wengine waliopo madarakani wamepandishwa vyeo, lakini
wanahusishwa na sakata hilo.
“Haiwezekani halmashauri kama hii kufanya ubadhirifu wa Sh bilioni 40 bila ya kushirikiana na Serikali Kuu,” alisema.
Kwa mujibu wa matokeo ya ukaguzi wa CAG, Halmashauri ya Jiji la Mwanza haikufanya vizuri katika maeneo ya uwekaji wa kumbukumbu za
hesabu zake, udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali na miradi maendeleo.
Aliongeza kuwa, licha ya halmashauri za mkoa wa Mwanza kupata hati zisizoridhisha, lakini ya Jiji pekee ndiyo iliyopata hati chafu.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula alisema hawezi kukubali ama kukataa juu ya ubadhirifu huo na kuhoji kuwa bajeti ya halmashauri ni Sh bilioni 6 na kuwa ubadhirifu wa Sh bilioni 40 ni kiasi
kikubwa cha fedha.
Akizungumzia kufutwa kwa halmashauri ya Jiji na kuwa Manispaa, alisema si sawa kwani kuwa Jiji ni kutoa wigo mpana wa maendeleo kwa wananchi
na kuwa wameshapita hadhi ya kuwa Manispaa.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Khalifa Hidda alisema hatokubali kuona hali hiyo ikiendelea na kwamba atachukua hatua na tahadhari zote.
Miongoni mwa fedha zinazodaiwa kutafunwa na Halmashauri ya Jiji ni pamoja na Sh bilioni 1.8
zilizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF) kwa ajili ya malipo ya fidia ya viwanja katika eneo la Bugarika ambapo halmashauri ilizifungulia akaunti bila kibali cha
Serikali.
Chapisha Maoni