0
TIMU kongwe za soka nchini, Simba na
Yanga zinashuka dimbani leo kumenyana katika mechi ya ligi kuu ya
Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo la watani wa jadi,
linasubiriwa kwa hamu kubwa na
mashabiki wa soka nchini kwa vile ndilo
litakalomaliza ubishi wa timu ipi bora
kati ya hizo msimu huu.

Simba itashuka dimbani huku
mwenendo wake katika ligi hiyo ukiwa
wa kusuasua baada ya kutoka sare katika
mechi zote tatu za mwanzo.
Katika mechi yake ya kwanza, Simba
ilitoka sare ya mabao 2-2 na Coastal
Union, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na
Polisi Moro kabla ya kulazimishwa sare
nyingine ya bao 1-1 na Stand United ya
Shinyanga. Nayo Yanga ilianza vibaya ligi hiyo baada
ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa
Sugar, lakini ikazinduka katika mechi
mbili zilizofuata baada ya kuichapa
Prisons mabao 2-1 na kisha kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1.
Katika mechi hiyo, Simba huenda
ikawakosa makipa wake wawili, Ivo
Mapunda na Hussein Sharifu 'Casillas'
kutokana na kuwa majeruhi, hali
inayomchanganya Kocha Mkuu wa timu
hiyo, Patrick Phiri.
Iwapo makipa hao watashindwa
kushuka dimbani, tegemeo pekee la
Simba litakuwa kwa kipa wake chipukizi,
Manyima Peter, ambaye ni mtoto wa
kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika.
Ivo alivunjika kidole cha mkono wiki
mbili zilizopita wakati Sharifu ameumia
kifundo cha mguu na atakuwa nje ya
uwanja kwa miezi sita.
Hata hivyo, Phiri alisema taarifa za
madaktari waliomtibu Ivo zimeeleza
kuwa, huenda kipa huyo akawa fiti kabla
ya mechi ya kesho.
Katika kujiandaa na mechi hiyo, Simba
ilikwenda kuweka kambi ya siku 10
nchini Afrika Kusini na pia kucheza
mechi tatu za kirafiki, ambapo ilichapwa
mabao 2-0 na Jomo Cosmos, ilifungwa
mabao 4-2 na Bidvest Wits na kutoka
suluhu na Orlando Pirates.
Kwa upande wa Yanga, wachezaji wake
Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kevin
Yondan, ambao walikuwa majeruhi, kwa
sasa wapo fiti na wameanza mazoezi ya
pamoja na wenzao.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio
Maximo amesema wachezaji wake wote
wapo fiti na wana ari kubwa ya kushinda
mchezo huo ili kulinda heshima yao.
Pambano hilo litachezeshwa na
mwamuzi Israel Nkongo, ambaye Yanga
iliandika barua kwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), ikilalamika kwamba
haina imani naye na kutaka abadilishwe.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Waamuzi ya TFF, Salum Umande alisema
jana kuwa, wameamua kuyatupilia mbali
maombi hayo ya Yanga kwa sababu
hayana mashiko.
"Yanga waliandika barua ya
kumlalamikia Mkongo katika mechi zao,
lakini sisi tunachoangalia ni jinsi gani
mwamuzi anatafsiri vyema sheria 17 za
soka na katika hilo, Nkongo analimudu
vyema,"alisema.
Hata hivyo, Umande alisema wameamua
kumbadilisha mshika kibendera
Ferdinand Chacha wa Mwanza, ambaye
nafasi yake sasa itachukuliwa na Samuel
Mpenzu kutoka Arusha. Mshika
kibendera mwingine katika mechi hiyo
atakuwa John Kanyenye kutoka Mbeya.

Chapisha Maoni

 
Top