0
Mkutano wa 36 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi wanachama wa SADC (SADC PF) ulioanza wiki hii mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe na unatarajiwa kumalizika tarehe 3 Novemba, 2014, ikiwa ni baada ya kukamilika kwa ajenda ya Mkutano huu pamoja na kufanyika kwa uchaguzi wa Rais wa chama hicho atakayeongoza jukwaa hilo
kwa miaka miwili ijayo.

Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Bunge la
kikanda la SADC – Wakati ni huu” ama
kwa lugha ya kimombo inasema “ SADC
Regional Parliament – the Future is Now”. Maneno yaliyo katika kauli mbiu ya Mkutano huu yamebeba ujumbe mzito sana
wa Mabunge ya Nchi za SADC ikiwa ni
dhamira ya dhati waliyokuwa nayo
wanachama hawa ya kuundwa kwa Bunge la kikanda litakalokuwa na nguvu si tu ya kuzisimamia Serikali za Nchi Wanachama
bali pia kuwa na uhalali wa kuhakikisha
kuwa maamuzi na hata mikataba
mbalimbali itakayofikiwa na chombo hiki
katika ukanda huu vinatekelezwa katika
nchi wanachama.

Pamoja na kwamba yapo mengi
yaliyojadiliwa katika Mkutano huu wa
Umoja wa Mabunge ya SADC hapa
Zimbabwe, muhimu limekuwa ni uchaguzi wa Rais wa Jukwaa hili ambaye ataongoza
jitihada za kufanikisha malengo ya chama hiki ya kufikia kuwa Bunge kamili ndani ya Miaka miwili ijayo yanafanikiwa.
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne
Makinda amekuwa akipigiwa chapuo na
Wajumbe wengi wa Mkutano ili aweze
kukamata usukani wa kukiongoza chama hiki kwa miaka miwili ijayo baada ya Rais wa sasa ambaye pia ni Spika wa Mauritius
Mhe. Abdool Razack Mahomed Ameen
Peeroo, kumaliza muda wake. Kutokana na
uungwaji mkono mkubwa alionao Mhe.
Makinda ameibuka kuwa mgombea pekee na hivyo ni dhahiri atapitishwa na
kukabidhiwa jukumu la kuongoza Jukwaa hili.
Msukumo wa Wajumbe wa Mkutano huu wa 36 kutaka Spika Makinda aweze kuongoza Bunge hili unatokana na heshima na
ushawishi mkubwa ilivyonayo nchi ya
Tanzania katika nchi wanachama wa SADC swala ambalo linafanya wajumbe wengi wa Umoja huu waamini kuwa Mtanzania
Makinda atasaidia sana kusukuma
masuala ya Jukwaa hili kwa Wakuu wa
nchi wanachama, kazi ambayo inahitaji
mtu kutoka nchi inayokubalika na yenye
sifa za kidemokrasia ya kweli kwa na hivyo kuweza kupenyeza na kufanikisha matakwa ya Bunge hili.
Kukubalika kwa Tanzania katika Ukanda
wa huu wa Afrika Kusini na chapuo
anayopigiwa Makinda ya kuongoza Bunge la SADC vinatokana na historia
iliyoandikwa na Tanzania kupitia harakati
za Ukombozi wa Bara la Afrika kuanzia
mwanzoni mwa miaka ya 1960. Kuanzia
wakati huo nchi ya Tanzania chini ya
Uongozi wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, iliongoza
mapambano ya ukombozi Barani Afrika na kutoa msaada mkubwa kwa Vyama
vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa
Afrika kama vile, Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC naPAC), Namibia (SWAPO), An gola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo). Uchaguzi wa Rais wa Umoja huu unafanyika tarehe 2 Novemba, 2014. Kwa
taratibu za Jukwaa hili la Kibunge, nafasi
hii hushikwa kwa kuzunguka kwa zamu
miongoni mwa nchi wanachama. Kwa
mzunguko huo hivi sasa ni zamu ya
Tanzania, Msumbuji, na Seychelles kuweka mgombea.
Licha ya kwamba nchi tatu zina nafasi ya kusimamisha wagombea, tayari wajumbe wa mkutano kutoka mabunge mbalimbali
za SADC wamekuwa wakifanya jitihada za Makusudi ili Spika Makinda aweze kupewa nafasi hii waweze kutumiza malengo waliyokuwa wamejiwekea.

Makinda sio kwamba ni mgeni katika
Umoja huu, ushawishi unaojitokeza na
wajumbe hawa pia unasukumwa na
mafanikio makubwa yaliyopatikana huko
nyuma katika kipindi alichoshika nafasi ya Makamu kuanzia mwaka 2008 hadi 2010 akiwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania.
Katika kipindi hicho, Makinda aliweza
kushirikiana na Rais wa Chama hicho
kuhakikisha kuwa nguvu ya umoja huu
hususani katika kukuza uwajibikaji na
demokrasia katika nchi wanachama
inakuwa kubwa. Aidha, ni katika kipindi
hiki ambapo Wabunge wengi kutoka nchi
wanachama waliweza kushiriki zoezi la
Uangalizi wa Chaguzi kwa lengo la
kuangalia kiwango cha Demokrasia katika nchi zilizokuwa na uchaguzi.

Pamoja na kuwa Makinda alishawahi kuwa Makamu wa Rais wa chama hiki, pia ndiye aliyeongoza zoezi la uangalizi wa uchaguzi katika uchaguzi Mkuu wa Botswana mwaka
2009.
Moja ya mambo makuu anayokumbukwa nayo wakati wa uongozi wake ilikuwa ni pamoja na kuongoza ujumbe wa Wabunge
wanawake kutoka nchi za SADC kwenda
katika nchi za Botswana, Malawi, Msumbiji na Zambia kwa lengo la kushawishi Mataifa hayo kuongeza idadi ya uwakilishi wa wanawake katika mabunge yao kuweza
kufikia angalau asilimia 30.

Uchaguzi wa Rais wa chama hiki mwaka
huu, unakuja kukiwa na matarajio
makubwa ya kuwa na Bunge madhubuti la SADC ambapo Katibu Mkuu wa umoja huu Dkt. Esau Chiviya, anasema kauli mbiu ya mwaka inazingatia na kuhitimisha matarajio ya waasisi wa umoja huu ya kuwa na Bunge imara la ukanda huu wa SADC ambapo anaamini kuchaguliwa kwa Rais kulenge kwenda sambamba na uwezo
wa kuweza kufanikisha jambo hili haraka iwezekanavyo.

Kuanzishwa kwa Umoja wa Mabunge
wanachama wa SADC kulifanikiwa tangu
tarehe 8 Septemba, 1997, mjini Blantyre,
Malawi, baada ya wakuu wa Nchi za SADC kupitisha azimio la kuanzishwa kwa Umojabhuu ikiwa ni jitihada za kuelekea kuwa na Bunge la Ukanda litakalo kuwa na majukumu ya kujadili masuala ya kibunge
na yenye maslahi ya ukanda huu katika
ngazi ya kibunge
Ni dhahiri sasa watanzania tuna kila
sababu ya kumuombea Makinda aweze
kupitishwa kuwa Rais wa Umoja huu ili
aweze kutimiza ndoto ya wanachama wa
Umoja wa Mabunge ya SADC ikiwa ni
pamoja na kuendelea kuiletea heshima
Tanzania katika nyanja ya kimataifa.
Mataifa mengi duniani hujitahidi sana
kuhakikisha kuwa viongozi na wananchi
wao wanashika nafasi mbalimbali kubwa
katika vyombo vya kimataifa ili kuendelea
kuyatangaza majina ya mataifa yao.
Tanzania hatuna budi kupiga chapuo
jitihada hizi kwa lengo la kuongeza
ushawishi wetu katika masuala ya
kidiplomasia.
Kwa hivi sasa Rais Robert Mugabe ndiye
mwenyekiti wa wakuu wa nchi za SADC. Ni
mtarajio kuwa baada ya uchaguzi wa
Makinda katika Mkutano huu, atasaidia
kuendelea kumshawishi Rais Mugabe kuwa
sasa nia na matarajio ya Umoja huu
yaliyokuwepo tangu kuanzishwa kwake ili liwe Bunge madhubuti katika Ukanda huu linakuwa moja ya ajenda kuu katika
Mkutano ujao wa wakuu wa Nchi za SADC unaotarajiwa kufanyika Mwakani 2015 nchini Botswana.

Umoja huu wa Mabunge kutoka SADC
ulianzishwa mwaka 1996 na malengo
makuu yake ni kujadili na kufanikisha
masula ya kibunge yenye maslahi kwa
wananchi ukanda huu na ikiwa ni sehemu
ya Wawakilishi hawa wa wanachi
kubadilishana uzoefu ambapo katika
mikutano yake kila Bunge huwakilishwa na
ujumbe usiozidi wabunge sita ikiwa ni
pmaoja na Maspika wao na uwakilishi ni
sharti uzingatie jinsia na uwakilishi wa
vyama uliopo katika Bunge.
Kwa upande wa Tanzania, Makinda
anaongoza ujumbe wa Wabunge watano
ambao ni Mhe. Seleman Jafo, Mhe. Anna
Abdalah, Mhe. Mohamed Mnyaa, Mhe.
Goodluck Ole-Medeye, na Mhe. Stella
Manyanya.
Zaidi ya Wabunge 100 ikiwa ni pamoja na Maspika wa Mabunge ya kutoka nchi za Angola, Democratic Republic of Congo
(DRC), Lesotho, Malawi, Namibia,
Seychelles, Afrika Kusini, Swaziland,
Tanzania, Zambia na Wenyeji Zimbabwe
wanashiriki Mkutano huu.
Ni wabunge kutoka Mauritius na Botswana tu ambao kwa sasa hawajaweza kushiriki kutokana na kuwa Mabunge yao yalivunjwa
kupisha uchaguzi mkuu katika nchi zao.
Kama Mtanzania na sote kwa pamoja
tuunge mkono Spika Makinda kushika
nafasi ya Rais wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za SADC. Kila la kheri Spika Makinda,

Chapisha Maoni

 
Top