0
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola.


Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4), ameibiwa nyumbani kwao katika kijiji cha Ndami, Tarafa ya Mwamashimba, Wilaya
ya Kwimba, mkoani Mwanza, akiwa amelala na wazazi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 27, mwaka huu saa 4:30 usiku, baada ya watu
hao kuvunja mlango wa nyumba kwa kutumia jiwe kubwa, maarufu kama ‘fatuma’ na kuingia ndani.

“Huyu mtoto akiwa amelala na baba yake, Emmanuel Shilinde, watu wawili walivamia nyumba hiyo na kuwaweka chini ya ulinzi wote waliokuwamo na kisha kumbeba mtoto huyo na kutoweka naye kusikojulikana,” alisema Mlowola.

Alisema watu hao baada ya kumchukua mtoto huyo, waliondoka kwa kasi wakitumia pikipiki na kutokomea kusikojulikana.

Mlowola alisema polisi walipata taarifa za tukio hilo saa 7:00 usiku baada ya kupigiwa simu na kuanza msako wa kumtafuta mtoto huyo pamoja
na watuhumiwa hao.

“Polisi wa Wilaya ya Kwimba, Misungwi na Mwanza, walianza msako baada ya taarifa hizo, lakini mpaka sasa tunawashikilia watu wanne, akiwamo baba wa mtoto huyo, Shilinde,” alisema
Kamanda Mlowola.

Hata hivyo, Mlowola alisema kikosi kazi cha upelelezi kutoka makao makuu ya polisi jijini Dar es Salaam, kimewasili jijini Mwanza kwa ajili ya kushirikiana na waliopo ili kumsaka mtoto huyo
akiwa hai au amekufa pamoja na walioshiriki wizi huo.

Alisema katika mazingira ya kawaida katika kijiji hicho, tukio hilo haliwezi kufanywa bila kuwapo na wenyeji, hivyo kwa uchunguzi wa awali wanawashikilia watu hao wanne, kulisaidia jeshi
hilo kwa upelelezi.

Mlowola alisema matukio ya mauaji ya albino katika mkoa huu, yalipungua kwa kiasi kikubwa na katika kipindi cha mwaka huu hilo ni la kwanza
kutokea.

Na kwa mikoa inayozunguka kanda ya ziwa, matukio hayo yamepungua kwa kasi kubwa baada ya kuimarishwa kwa ulinzi na kuwanasa watuhumiwa waliokuwa wakiyafanya yanayoaminiwa zaidi ni kwa ajili ya imani za
kishirikina.

Alisema matukio ya mauaji ya albino katika mikoa hiyo, ni manne tu yametokea katika mikoa ya
Tabora, Shinyanga, Simiyu na Mwanza, hali inayoonyesha kupungua kwa kasi kubwa.

Mauaji ya albino yamekuwa ni tatizo kubwa nchini hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Pamoja na serikali kutangaza hatua kadhaa za kupambana na wauaji hao, bado matukio ya kuuawa albino yamekuwa yakiendelea kuripotiwa.

Chapisha Maoni

 
Top