0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza mwanamuziki Nassib Abdul maarufu kwa jina la Diamond na Mshindi wa Shindano la Big Brother
Africa, Idris Sultan kwa kuiletea sifa Tanzania kupitia sanaa.

Rais Kikwete ametoa Pongezi hizo alipokutana na Msanii Diamond Ikulu jijini Dar es salaam Jumanne Desemba 23, 2014 , ambapo Msanii huyo amemwonyesha tuzo tano alizoshinda baada ya kupambanishwa na wasanii wengine wa Afrika.

Pamoja na pongezi hizo kwa Diamond na Idris kwa kile alichosema wameitoa nchi kimasomaso, Rais Kikwete amewasihi wasanii hao kujihadhari
na athari za umaarufu na utajiri katika umri mdogo,zikiwemo kujitumbukiza katika matumizi ya dawa za kulevya na ulevi.

Kikwete amewaasa kuwa ni muhimu kwa wasanii hao kutumia mapato wanayoyapata katika kazi zao za usanii kwa kujijenga kifamilia ikiwa ni pamoja
na kujenga nyumba zao za kuishi na wanafamilia wanaowategemea pamoja kuwasaidia wasanii wenzao.

“Umaarufu katika sanaa yoyote ile ni wa kupita hivyo tumieni umaarufu mlio nao sasa kama fursa ya kujijenga kimaisha na sio kutumbukia katika kadhia za kidunia kama vile ulevi, ukorofi mbele
ya jamii na mambo mengine yasiyofaa", aliwaasa Mhe. Rais.

Rais Kikwete pia alimpongeza Sultan kwa kuiletea Tanzania sifa na kumtakia mafanikio zaidi katika shughuli zake za baadaye. Rais Kikwete alisema kuwa Sultan hakuifedhehesha Tanzania kwa
kutofanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Mwafrika alipokuwa katika jumba la Big Brother Africa.

Kwa upande wake,Diamond amemshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa ushirikiano anaoutoa kwa wasanii hapa nchini, hali ambayo
amesema ndiyo iliyowawezesha kupata mafanikio kitaifa na kimataifa.

Diamond pia amemuahidi Rais Kikwete kutekeleza yote aliyomuasa kuhusu kujiheshimu na kutolewa umaarufu alionao, na kwamba ataendelea kufanya
kazi zake za usanii wa Muziki kwa juhudi zake zote kuitangaza nchi.

Msanii huyo pia amemweleza Rais Kikwete kuwa hivi karibuni atapokea tuzo nyingine ya sita kutoka huko Nigeria.
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo toka kwa msanii Naseeb Abdul “Diamond” wakati akimuonesha moja ya tuzo kati ya tuzo tano za muziki za kimataifa alizoshinda mwaka huu, Ikulu
jijini Dar es salaam Jumanne Desemba 23, 2014.

kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni Katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Hermas Mwansoko.
 Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo toka kwa msanii Naseeb Abdul “Diamond” juu ya ushindi wake wa tuzo tano za muziki za kimataifa mwaka huu, Ikulu jijini Dar es salaam Jumanne
Desemba 23, 2014
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akipokea CD mpya ya msanii Naseeb Abdul “Diamond” baada ya kuoneshwa tuzo tano za muziki za kimataifa alizoshinda mwaka huu, Ikulu jijini Dar
es salaam Jumanne Desemba 23, 2014.
Tuzo tano za muziki za kimataifa alizoshinda Naseeb Abdul “Diamond” mwaka huu 2014

Chapisha Maoni

 
Top