0
Ikiwa imebaki miezi 10 tu
kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu
mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na
tuhuma za rushwa inayodaiwa kutolewa
na makada wake wanaotajwa kutaka
kuwania nafasi mbalimbali ukiwamo
urais.
Hali hiyo inabainishwa na kauli za
baadhi ya makada wa chama hicho katika ngazi mbalimbali ambao wameamua kulalamika waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au kwenye mitandao ya kijamii.

Moja ya kauli hizo ni ile iliyotolewa juzi
na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi
Khamis Kagasheki kwenye akaunti yake
ya Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass
na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika
wa CCM ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo
wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake,
Kagasheki alisema kwenye maoni yake
hakutaja mtu licha ya kwamba wapo
wengi wanaotoa zawadi, lakini baada ya
kuandika katika mtandao ameandamwa
na baadhi ya watu huku wengine
wakimtolea lugha chafu.

“Hii ni line yangu ninaitumia kutoa
mawazo siku zote, lakini nimeshangaa
leo watu wameshikia kidedea maoni
hayo mpaka wengine wanatumia lugha
kali... sijamtaja mtu kwa sababu najua
wapo watu wengi wanaotoa zawadi,”
alisema Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii huku
akisisitiza kuwa hayo ni mawazo huru
ambayo anayaamini.

Waliyonena kuhusu rushwa
Kauli ya Kagasheki haina tofauti na zile
zilizowahi kutolewa na makada wengine,
akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete na wengine waliowahi kushika
nyadhifa za juu ndani ya chama hicho na
Serikali yake juu ya kukithiri kwa rushwa
katika kusaka madaraka.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip
Mangula alimwambia mwandishi wetu
jana kuwa suala hilo linafuatiliwa kwa
karibu na dawa yake itaiva Februari
baada ya kamati yake ya maadili
iliyofuatilia kutoa tathmini yake.
“Tulipotangaza kuwafungia, tuliunda
kamati ya ufuatiliaji harakati za kila
mmoja kuona je, yale tuliyomtaka
kutoyafanya ametekeleza? Sisi
tunaheshimu vikao vyetu, hivyo
tunasubiri kamati hiyo itakapotuletea
taarifa yake.

“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo
wa kusamehewa watasamehewa na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”
Kauli ya Mangula ilikuwa inafafanua
makada wa chama hicho waliopewa onyo
kali kwa kufanya kampeni mapema na
kujihusisha na vitendo vinavyokiuka
maadili ndani ya chama na ndani ya
jamii.

Mangula alisema hayo wakati kukiwa na
madai kuwa baadhi ya wanachama wake kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine
ya nchi.
Mangula jana alikaririwa na gazeti la
CCM, Uhuru, akijibu madai hayo kuwa,
“hakuna mwanachama aliye juu ya
katiba, kanuni na miongozo ya chama na
hivyo hakitamvumilia mtu yeyote
atakayebainika kutumia fedha.”
Kwa mujibu wa madai hayo, kada mmoja
wa CCM anadaiwa kugawa kati ya Sh1
milioni na Sh500,000 kama zawadi ya
sikukuu ya Krismasi kwa wajumbe wa
vikao vya chama visiwani humo.
Mangula alisema kutokana na
malalamiko hayo, CCM itapeleka timu ya
uchunguzi kupitia kitengo cha usalama
na maadili kuchunguza tuhuma hizo.
Oktoba 25, mwaka jana Rais Kikwete
alisema endapo rushwa haitakomeshwa
ndani ya CCM, kitaanguka vibaya katika
Uchaguzi Mkuu 2015 na iwapo
kitanusurika hakitapita mwaka 2020.
Kauli hiyo pia inaungwa mkono na
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
aliyewahi kuliambia gazeti hili kuwa
iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM
itaendelea kulalia kwenye rushwa,
hataendelea kuwa sehemu yake na
kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya
na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete alitangaza
mkakati wa ‘kujivua gamba’ akiwataka
makada wa chama hicho
wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari
na kujiondoa ndani ya siku 90, lakini hata
baada ya muda huo kumalizika, mkakati
huo uliyeyuka na viongozi wakaanza
kubadili maudhui yake.
Waliopigwa ‘stop’
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wasira, Naibu Waziri
wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba na aliyewahi kuwa
Waziri wa Nishati na Madini, William
Ngeleja.
Wanavyoitazama CCM
Wachambuzi waliozungumza na gazeti
hili walisema CCM hakiwezi kupambana
na rushwa kwa sababu baadhi ya
viongozi wake ni walarushwa na
wamekiondoa katika misingi ya
kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Bashiru Ally alisema: “Chama
hakiongozwi kwa makaripio, mkakati wa
kujivua gamba na matamko katika
vyombo vya habari. Kinaongozwa kwa
mifumo imara, fikra sahihi, dira na
historia yake nzuri.
“Ndiyo maana wanachama wa CCM
wamekuwa wakitenda mambo kinyume
na katiba ya chama chao na hakuna wa
kuwachukulia hatua. Kolimba
(marehemu) aliwahi kusema kuwa CCM
haina dira wala mwelekeo. Hilo
linaonekana sasa, kimeshindwa kukemea
rushwa.”
Alisema ni vigumu kwa CCM kuikataa
rushwa wakati baadhi ya wanachama
wake, tena wenye nyadhifa za juu ndani
ya chama hicho wakituhumiwa kwa
rushwa.
“Mchawi yupo ndani ya CCM yenyewe.
Profesa Tibaijuka ni mjumbe wa Kamati
Kuu na amepewa mgawo wa escrow
lakini chama kipo kimya. Jimbo la
Bukoba Vijijini limegawanyika kwa
sababu ya rushwa inayotolewa na
wanaotaka ubunge, hayo yote CCM
hawayaoni na kukimbilia yanayotokea
Zanzibar,” alisema. Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es
Salaam, Dk Benson Bana alisema: “CCM
ni chama ambacho kinajibu mapigo ila
hakitoi mapigo. Kinachotokea sasa ni
dalili mbaya kwake kwani kimekuwa
dhaifu katika kuwashughulikia
wanachama wake wasio waadilifu.”
Alisema matamko mengi ya chama hicho
ni ya kisiasa zaidi na mengi huishia
katika vyombo vya habari. “Hayo
yanamaanisha kuwa uwezo wa CCM
umepungua. Mfano ni Chadema kwa sasa
kinatoa mapigo na si kujibu mapigo
pekee. Hiyo ndiyo inatakiwa kufanywa na
chama cha siasa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa alisema Mangula alipotangazwa
kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM
aliahidi kupambana na rushwa na mpaka
leo kashindwa.



Africa Newss
Mwananchi

Chapisha Maoni

 
Top