0
Mfanyabiashara wa mbao Manispaa ya Songea, Emmanuel Moshi (40), mkazi wa Marangu, mkoani Kilimanjaro amemuua mfanyabiashara mwenzake
aliyetambuliwa kwa jina la Didas Alphonce (64), mkazi wa Kilema Kilimanjaro kwa kumpasua
kichwa kwa shoka, kisha yeye mwenyewe kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani katika stoo ya nyumba waliyokuwa wakiishi.

Inadaiwa kuwa Moshi alichukua uamuzi huo baada ya Alphonce kumdhulumu zaidi ya Sh87.4 milioni.
Wakizungumza na Mwandishi jana, watu wa karibu na wafanyabiashara hao ambao hawakupenda majina yao kuandikwa, walidai kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakiishi nyumba ya ndugu yake, Didas na kufanya biashara za kuuza mbao pamoja.

Walidai kuwa, Desemba 30 mwaka jana,
wafanyabiashara hao walikuwa wakinywa pombe kwenye Bwalo la Magereza na Moshi alikuwa
akilalamika kudhulumiwa na Didas.
Mashuhuda hao waliongeza kuwa tangu siku hiyo, wafanyabiashara hao hawakuonekana tena hadi
jana.

Ilidaiwa kuwa, mwenye nyumba huyo alitumia funguo zake za akiba kufungua nyumba hiyo na kukuta mwili wa mjomba wake ukiwa umepigwa
na shoka na tayari umeanza kuharibika.
Mtu mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi alitoa taarifa kituo cha polisi na walipofika waliubaini pia
mwili wa Moshi aliyejinyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai uchunguzi wa awali unaonyesha wafanyabiashara hao walikuwa wanadaiana pesa.

Alisema Mosha ameacha ujumbe mrefu wa karatasi nne aliouandika kuhusiana na mauaji hayo.

Ujumbe huo: “Kataeni wadhulumaji kati ya matajiri na maskini, nimeondoa dhambi kubwa ya dhuluma iliyokuwa ikinitesa ulimwenguni, wadhulumaji wasifumbiwe macho jamii iniunge
mkono kuondoa watu hawa.
“Dhuluma aliyonifanyia mtu huyu imekatisha maisha yangu.”

Chapisha Maoni

 
Top