BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeendeleza msimamo wake wa kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM,
uliopangwa kufanyika Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma.
Katika kuhakikisha linatimiza azma yake hiyo, baraza hilo limesema wanachama wake wapatao
4,000 wamejiandaa kushiriki kwenye shughuli
hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, baada ya kuhojiwa kwenye Kituo
Kikuu cha Polisi, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha,
Patrick ole Sosopi, alisema kuna vijana
watakaotoka sehemu mbalimbali ili kuzuia
mkutano wa CCM.
Sosopi alisema Bavicha watakwenda Dodoma
kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kile
walichodai kusaidia Jeshi la Polisi kutekeleza
amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi
2020.
Alisema pia kuna watu wamejitolea kutoa magari
kwa ajili ya kuwabeba vijana hao ili kuwafikisha
Dodoma kuunga mkono agizo la polisi.
Sosopi pia aliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia
hatua viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) kutokana na kauli zao za vitisho
walizozitoa dhidi ya Bavicha hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4,
mwaka huu, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka
Hamad Shaka, aliionya Bavicha wasiende Dodoma
kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kuwa
watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda
heshima ya chama chao.
Sosopi alisema wao hawataki matatizo wala
vurugu bali wanachofanya ni kutii agizo la polisi
kwa unyenyekevu.
"Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu
kwani Rais alipopiga marufuku mikutano ya
kisiasa hadi 2020, CCM walichekelea wakiamini
kuwa Chadema tumekomolewa lakini iweje sasa
Jeshi la Polisi likubali kuruhusu mkutano wao
wakati Chadema hata mikutano ya ndani
tunazuiliwa?
"Hatutanii hata kidogo na wala CCM wasidhani
kuwa hatutakwenda Dodoma lakini tunaliomba
Jeshi la Polisi litende haki juu ya kauli za
uchochezi kwani nilitegemea viongozi wa UVCCM
wangekamatwa na jeshi hilo lakini tunaokamatwa
ni sisi tu," alisema Ole Sosopi.
Akizungumzia suala la kuhojiwa na polisi jana,
Ole Sosopi alisema alikuwa kituoni hapo kuhojiwa
kwa kosa analodaiwa kufanya Juni 18, mwaka
huu la kutoa kauli za uchochezi.
Sosopi alikamatwa mara ya kwanza Juni 26,
mwaka huu mkoani Iringa na kusafirishwa hadi
jijini Dar es Salaam na
kuhojiwa kwa kosa hilo katika shughuli ya
mahafali ya wanachama wa Chadema waliomaliza
vyuo vikuu.
Sosopi alisema baada ya kuhojiwa jana na polisi,
anatakiwa kuripoti tena kituoni hapo Julai 18,
mwaka huu.
Akizungumzia suala la Sosopi, mwanasheria
wake, Frederick Kihwelo alisema Sosopi aliripoti
kituoni hapo kwani anakabiliwa na tuhuma ya
kutoa lugha ya uchochezi.
Alidai lengo la mteja wake ni kuhakikisha polisi
wanatenda haki bila upendeleo kwani kazi yao kubwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao
Alisema baada ya kuhojiwa na polisi jana,
atatakiwa kufika tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu wakati huu upelelezi unafanyika na
ushahidi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaki
ya Jinai (DPP) ili aamue kama kuna kesi ya kujibu au la.
Chapisha Maoni