0
Rais John Magufuli amemwaga burungutu la fedha kusaidia Waislamu ambao watakwenda
kuhiji Agosti mwaka huu.
“Najua kuna Waislamu watakwenda kuhiji nadhani
Agosti, naomba kama inaruhusiwa na mimi
nichangie kitu kidogo kadri ya uwezo wangu,
nimejipigapiga na mimi nikaona nichangie kitu
kidogo, kana inaruhusiwa naomba Mufti uje
nikukabidhi,” alisema Magufuli alipokuwa
akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri jijini Dar
es Salaam jana.
Baada ya kutamka maneno hayo, alishika begi
dogo kama briefcase akampa msaidizi wake
ambaye alilifungua na kuchomoa burunguti la noti
na kumkabidhi Mufti, Sheikh Mkuu Zubeiry Ally.
Hata hivyo haikufahamika kiasi cha fedha hizo.
Kabla ya kutoa fedha hizo, awali akimkaribisha
Rais Magufuli kuhutubia, Mufti Zubeiry aliwataka
Waislamu kutumia Bakwata katika safari za hija
zitakazogharimu Dola 3,800 kwa mtu mmoja.
Awali Magufuli alikuwa ameahidi kitita cha Sh2
milioni kwa kijana aliyesoma dua katika sherehe
hizo pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa
kundi la Kaswida lililotumbuiza.
Katika hotuba yake, Dk Magufuli alisema Serikali
yake ipo katika mchakato wa kurejesha heshima
yake ingawa kuna watu wachache watakaoguswa
kwa kuisababishia hasara Serikali.
Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika
baraza hilo la Eid el Firti alisema Tanzania ni nchi
tajiri lakini baadhi ya watu wamesababisha watu
waendelee kuwa masikini.
“Tanzania hii ni tajiri sana, kila kitu kipo. Juzi
mpaka wamegundua Helium tani za kutosha. Kila
madini yapo hapa. Lakini kwa nini tuko masikini?
Kwa nini watu wana shida? Ndiyo maana
tumeamua kwa niaba yenu turudishe heshima
yetu. tulete mabadiliko ya kweli na katika kufanya
hayo wapo watu watakaoguswa, lakini ni
wachache sana kuliko wale waliokuwa
wanaguswa kwa kuibiwa, ni wachache waliokuwa
wanadhulumiwa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kwa miezi saba tangu alipochaguliwa
kuingia madarakani Serikali yake imetekeleza
mambo kadhaa ikiwa pamoja na kutoa elimu bure
kwa shule za msingi na sekondari, kurudisha
nidhamu ya watumishi wa umma, kudhibiti
matumizi mabaya ndani ya Serikali, kuongeza
mapato na mengineyo.
“Pamoja na hatua hizo ni dhahiri kuwa bado tuna
safari ndefu katika kutimiza yale tuliyokusudia na
tuliyowaahidi Watanzania. Naomba
niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwahudumia
kwa nguvu zetu zote pamoja na vipaji vyote bado
tunayo. Tuna sababu ya msingi na tuna imani
kuwa Mungu yupo kuhakikisha kuwa tunaipeleka
nchi yeti mbele...” alisema Rais Magufuli huku
akiwataka waumini hao kuiombea Serikali.
Aliwataka viongozi wa dini ya Kiislamu
kuwahimiza waumini wao kushiriki katika
shughuli za maendeleo hususani katika
kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano ambao utekelezaji wake umeanza mwezi
huu.
“Tusipofanya kazi hatutapata pesa. Ndiyo maana
wale waliozoea kupata fedha za bure wameanza
kusema fedha zimeisha mifukoni. Hela haiji bila
kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu mali za Waislamu zilizodhulumiwa, Rais
Magufuli alisema atawasaidia kuzirejesha.
Alimpongeza Mufti wa Baraza la Waislamu
Tanzania (Bakwata), Zubeiry akisema alikuwa
mstari wa mbele katika kurejesha mali hizo kabla
hata hajapewa cheo hicho.
“Nakumbuka wakati nikiwa Waziri wa Ardhi, kabla
hujawa Mufti, pamoja na viongozi wa Bakwata na
wengine, ulifika ofisini kwangu ukieleza jinsi mali
za Waislamu zilivyokuwa zinadhulumiwa.
"Ninafamu pamekuwa na hiyo tabia ya baadhi ya
viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa
Bakwata na dini nyingine katika kuwarubuni na
kuingia ubia, mali hizo baadaye huwa zinapotea
kabisa,” alisema na kuongeza:
“Tujitahidi kwa nguvu zote kusimamia mali hizi,
zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani.
Tunapenda wawekezaji lakini wanachokiahidi
hawatekelezi, haiwezekani.
"Haiwezekani na wala haikubaliki kwa watu kwa
ujanja wao na wakati mwingine kwa kutumia
wanasheria wao kukalia mali za Waislamu. Mali
za Waislamu lazima zirudi na za Wakristo zirudi
ili amani iwepo.”
Baraza hilo lilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
Katibu wa Bakwata Sheikh Suleiman Lolila na
mabalozi wa nchi mbalimbali na waumini wa dini
hiyo.

Chapisha Maoni

 
Top