0
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la
Polisi kama lina nia ya kumkamata na kumweka
ndani lifanye hivyo kwa kuwa yeye yupo nchini.
Akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri
lililofanyika katika ukumbi wa Wakfii wa Ngazija
mjini Zanzibar, tofauti na jingine lililofanyika
ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani na
kuhutubiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein, Maalim Seif alisema nchi inapita katika
kipindi kigumu kutokana na dhuluma
inayotendwa na watawala dhidi ya raia wasiokuwa
na hatia.
“Huwezi kuamini kuwa dhuluma hii inatendwa na
watawala Waislamu. Hali ni mbaya, wananchi
wanapata hilaki kubwa baada ya hao wanaojiita
Serikali kubaini kuwa hawakubaliki.
"Mambo hayo yanafanywa kutokana na
kushindwa kuzigeuza nyoyo za wananchi ndiyo
maana wanafanya hujuma, vitendo vya kikatili na
kuwatisha wananchi,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alieleza kusikitishwa na hali ya
kamatakamata dhidi ya viongozi mbalimbali wa
CUF katika ngazi za wilaya na majimbo na
kuwekwa ndani huku wakiteswa, kuadhibiwa na
kulazimishwa kukubali kushiriki katika vitendo vya
uhalifu ambavyo hawakuvitenda.
Alibainisha kuwepo mwendelezo wa kauli
zinazoashiria azma ya kutaka kumkamata yeye,
zinazotolewa na baadhi ya wakuu wa vyombo vya
dola.
“Hakuna haja ya kuwatesa watu, iwapo wanayo
azma ya kunikamata, mimi nipo waje tu
wanikamate,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema vitendo vyote hivyo ni
mwendelezo wa dhuluma aliyoitenda Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha
Salim Jecha, tarehe 28 Oktoba 2015 wakati
akifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kabla ya
kuitisha ule wa marudio wa Machi 20.
Hii ni mara ya kwanza mpasuko wa kisiasa
unawaathiri Wazanzibari hata wakati wa Sikukuu
ya Eid -El Fitr inayoadhimishwa baada ya
kumalizika mfungo ya Mwezi Mtukufu wa
Ramadhan.
Akihutumia Baraza lililofanyika katika ukumbi wa
Baraza la Wawakilishi la zamani, Dk Shein
aliendelea kukazia kuwa Zanzibar haitakuwa na
uchaguzi mwingine mpaka mwaka 2020 kwa
kuwa Serikali iliyochaguliwa na wananchi
imeshaundwa.
Katika hotuba hiyo ya takriban dakika 35, alisema
hakutakuwa na Serikali ya mpito na kueleza kuwa
hayo “yanayosemwa mitaani ni maneno ya
wababaishaji.”

Chapisha Maoni

 
Top