0
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi mkuu visiwani humo ulishamalizika na hakuna mpango wa kuwepo kwa serikali ya mpito.
Amesema uchaguzi umekwisha kabla ya
mwingine utakaofanyika mwaka 2020; hivyo kazi
kubwa inayofanywa sasa ni kusimamia na
kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ya mwaka 2015-2020 kwa ajili ya kuwaletea
wananchi maendeleo.
Alisema hayo jana wakati akihutubia Baraza la
Iddi na kusisitiza kuwa atapambana na watu
ambao wamekuwa wakifanya mbinu serikali
ishindwe kutekeleza mipango yake.
Alisema wapo watu wamekuwa wakijaribu kufanya
mbinu na vituko serikali ishindwe kutekeleza
mipango yake, ikiwemo kusimamia ilani ya chama
na bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/2017.
Dk Shein aliwapongeza wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kwa kupitisha bajeti ya serikali kwa
mwaka wa fedha 2016/2017, ambayo kazi kubwa
itakayofanywa ni kusimamia mapato na kupata
fedha za kutekeleza mipango hiyo.
“Wananchi napenda kusema tena kwamba
uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine
ifikapo mwaka 2020...wanaotaka kuwepo kwa
serikali ya mpito wasahau,” alisema.
Alisema hakuna sababu ya kuwepo kwa serikali
ya mpito kwa sababu CCM ilishiriki katika
uchaguzi wa marudio na kushinda kwa kishindo.
Aliwataka wananchi kupuuza propaganda
zinazotolewa na wapinzani kwa ajili ya kile
alichosema ni kuwazubaisha wananchi washindwe
kufanya kazi zao vizuri.
Alikemea matukio yanayojitokeza zaidi katika
kisiwa cha Pemba, yakiashiria uvunjifu wa amani
na utulivu.
Alivitaka vyama vya siasa kufanya kazi zao bila
ya kukiuka sheria zilizopo. Alisema vitendo vya
chuki na ufisadi ni kinyume na maagizo ya
Mungu.
“Nimesikitishwa sana na matukio yote ambayo
yamelitia aibu kubwa taifa letu kwani hayaendani
na mafunzo tuliyoyapata katika kipindi cha
swaumu...tunatakiwa kuacha kujenga kiburi na
ufisadi,” alisema.
Wakati huo huo, alikemea matukio ya vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo vya kuwadhuru
watoto, ikiwemo baadhi vilivyofanyika katika
kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema serikali imejizatiti kupambana na matukio
hayo, ikiwemo kuanzishwa kwa mahakama ya
watoto, itakayosikiliza kwa haraka kesi
zinazohusu kundi hilo.
Alitaka jamii kuwa tayari kutoa ushahidi mbali ya
vyombo vya sheria ikiwa ndiyo njia muafaka ya
kukomesha matukio hayo.
“Serikali tumejipanga kupambana na matukio ya
vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia lakini jamii
nayo iwe tayari kutoa ushahidi mbele ya vyombo
vya sheria,” alisema.
Kwa upande wake, Mufti wa Zanzibar, Shehe Mkuu
Saleh Kabi alimpongeza rais kwa ustahimilivu
katika kuongoza visiwa vya Unguja na Pemba
kwa utulivu mkubwa na hekima.
“Huo ndiyo uongozi bora uliotukuka wa kuongoza
nchi kwa kutumia busara na hekima japo unajua
wapo watu wanaofanya vitimbi,” alisema.
Sherehe za baraza la Iddi zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali, akiwemo Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais
mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal.

Chapisha Maoni

 
Top