0
Mzazi aliyejifungua watoto watatu kwenye Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini akazuiwa wodini
kutokana na kudaiwa gharama za matibabu, jana
aliruhusiwa kuondoka baada ya Waziri wa Afya,
Ummy Mwalimu kuingilia kati suala hilo.
Mzazi huyo, Stella Nnko (38) aliyefikishwa
Muhimbili kwa rufaa akitokea Hospitali ya Mnazi
Mmoja, alikuwa akidaiwa Sh540,595.
Kulingana na gazeti la Mwananchi, Waziri Ummy
aliagiza mama huyo apewe watoto wake na
kuruhusiwa na jana asubuhi katibu mkuu wa
wizara, Dk Mpoki Ulisubisya alimtembelea mzazi
huyo kabla ya kuondoka hospitalini hapo.
Mama huyo, Stella alimshukuru Waziri kwa
kuingilia kati suala hilo na kuwaomba wasamaria
wema kumsaidia katika matunzo ya watoto hao
kwa kuwa uwezo wake kiuchumi si mzuri.
Alisema hajawahi kuonana na baba wa watoto hao
tangu alipompa ujauzito, na yeye hana uwezo wa
kuwatunza.
“Ninayaendesha maisha yangu kwa kukaanga
mihogo, shughuli ambayo kwa sasa nitashindwa
kuendelea kuifanya kwa sababu ya kuwahudumia
hawa watoto,” alisema Nnko.
“Nyumbani nimemwacha mwanangu wa miaka
miwili na nusu na sina msaidizi wala ndugu.”
Stella anaishi Kivule, Ilala jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kuondoka Muhimbili, watoto hao watatu
walipewa chanjo ya kupooza, BCG ya kifua kikuu
na matone ya vitamin A.
Mtoto mmoja kati yao ni wa kiume na alizaliwa
akiwa na uzito wa kilogramu 2.8 wakati wa kike
wawili walikuwa na uzito wa kilo 2.5 na 2.1.
Akizungumzia sakata hilo, mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Umma cha MNH, Aminiel Aligaesha
alisema Stella alifikishwa hospitalini hapo Juni 29
mwaka huu kwa dharura akitokea Mnazi Mmoja na
kufanyiwa upasuaji Juni 30.
Lakini alikanusha taarifa kwamba MNH ilimzuia
kutoka, bali alipewa hati ya malipo ili ajiandae
kulipa, kinyume na kauli ya Stella kwamba
aliruhusiwa kuondoka na kupewa hati ya malipo na
alipoeleza kuwa hana uwezo, alizuiwa mpaka
atakapochangia huduma.
“Wakati Stella akipewa huduma na kusubiri
kuruhusiwa, alipelekewa gharama ya jumla ya
Sh477,131 ikiwa ni gharama ya kujifungua kwa
upasuaji na huduma zote alizozipata tangu
alipopokelewa, zikiwemo dawa na vitendanishi.
Hakuzuiwa, ila alipewa hati ya malipo ili ajiandae
kulipa,” alisema Aligaesha.
Alisema pamoja na hayo, Nnko amesamahewa
kulipa gharama zote za matibabu na tayari
amesharuhusiwa kwenda nyumbani.
Kuhusu suala la tozo kwa mama wajawazito,
Aligaesha alisema ni utaratibu ambao uliwekwa na
hospitali wa kuchangia huduma kwa kuwa tangu
wameanza mfumo huo dawa na vitendanishi
vimekuwa haviadimiki ikilinganishwa na hapo
awali.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha kila mgonjwa
anayekuja kutibiwa MNH anapata dawa na huduma
zote kwa gharama nafuu. Tunawaomba wananchi
kuchangia huduma zote za afya ili tuweze kupata
fedha na kutoa huduma kwa mfumo endelevu.
Ndiyo maana ndani kuna duka la MSD,” alisema
Aliagesha.
Alisema iwapo akitokea mgonjwa hana uwezo wa
kuchangia huduma, utaratibu wa kumuombea
msamaha unatumika na atapata huduma bila
malipo.
Maiti iliyozuiliwa
MNH pia ilidaiwa kuzuia mwili wa marehemu Hilda
Mbawala aliyefariki Juni 26 kutokana na ndugu
zake kushindwa kulipia gharama za Sh1.4 milioni,
lakini Aligaesha alikanusha madai hayo.
“Wakati marehemu akitibiwa, ndugu walikuwa
wanapewa taarifa na mwenendo wa matibabu ya
ndugu yao, ikiwamo kuhimizwa kuchangia
huduma,” alisema Aligaesha.
“Baada ya kifo hicho, ndugu wa marehemu
walipewa hati ya gharama ya matibabu ya Sh1.4
milioni ili wakajipange jinsi ya kulipa.”
Alisema ndugu hao walisema hawana uwezo wa
kulipia kiasi hicho cha fedha na Juni 30
waliwasiliana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii ili
wasaidiwe na baada ya majadiliano pande zote
mbili zilikubaliana kuwa walipe Sh800,000.
“Wakati makubaliano hayo yakiwa kwenye hatua za
kuidhinishwa na mamlaka husika, ndipo ndugu
walipokimbilia kwenye vyombo vya habari na
kulalamika kuwa hospitali imezuia mwili.
Ukweli ni kwamba wamelipa kiasi hicho cha
Sh800,000 na wamesamehewa deni la Sh
623,747.64 na mwili waliuchukua Julai 5,” alisema.



Mwananchi

Chapisha Maoni

 
Top