0

Paul Scholes alikuwa haongei sana wakati
anacheza soka, lakini siku hizi hashikiki. Anaongea
linalomjia rohoni. Hafichi kitu.
Anaongea anachokiamini. Na tayari amepasulia
dongo jingine kwa klabu yake ya Manchester
United katika uhamisho mkubwa wanaotarajiwa
kuufanya.
Man United inakaribia kuvunja rekodi ya uhamisho
wa dunia kwa kiungo, Paul Pogba kutoka Juventus
ambaye walimkuza wenyewe na kumruhusu
kwenda Juventus mwaka 2012 kabla ya kuibuka
kuwa staa mkubwa duniani kwa sasa.
Lakini Paul Scholes, mmoja kati ya mastaa
wanaoheshimika Old Trafford ameibuka na kudai
kwamba Pogba hana thamani ya kuwa mchezaji
ghali zaidi duniani kwa sasa na hayupo katika
kiwango sawa na Lionel Messi na Cristiano
Ronaldo.
“Alikuwa ni kinda mwenye kipaji sana, nilicheza
naye na nilijua ni kiasi gani alikuwa mzuri.
Alicheza timu ya kwanza mara moja au mara mbili,
lakini kwa uelewa wangu alitaka apewe pesa nyingi
sana wakati alipoondoka mwaka 2012,” alisema
Scholes.
“Kwa umri wake nadhani alikuwa anaulizia pesa
nyingi sana kwa mchezaji ambaye alikuwa
hajacheza kikosi cha kwanza. Ok, amekwenda na
kufanya mambo makubwa.
"Nadhani ameimarika sana kisoka. Alihitajika
kuimarika kama alitaka kuwa mchezaji wa thamani
ya Pauni 86 milioni.”
“Sidhani kama ana thamani ya Pauni 86 milioni.
Kwa aina hiyo ya pesa, unahitaji iwe kwa mtu
ambaye anaweza kufunga mabao 50 kwa msimu
kama Ronaldo au Messi.
Pogba hajakaribia kabisa thamani ya pesa hiyo,”
aliongeza Scholes ambaye kwa sasa anafanya kazi
ya uchambuzi wa soka.
Hata hivyo, wakala wa mchezaji huyo, Mino Raiola
amedai kwamba hajali sana suala la mteja wake
kuvunja rekodi kwa sababu alishawahi kufanya
hivyo kwa wateja wake wa siku za nyuma.
“Sijali suala la kuvunja rekodi za uhamisho.
Magazeti yanasema Pogba anaweza kuvunja rekodi
za uhamisho lakini tayari nilishavunja rekodi za
uhamisho na Ibrahimovic na Pavel Nedved.
Nafanya kile kilicho bora kwa wachezaji wangu na
hao ni pamoja na Pogba.”
“Je Pogba ameomba kuondoka Juventus? Sitajibu
swali hilo kwa mtu yeyote na siongei biashara
hadharani. Baadhi ya vitu huwa najadili na wateja
wangu tu na wanajua jinsi mambo yalivyo,”
aliongeza wakala huyo ambaye pia ni wakala wa
mshambuliaji mtukutu wa Liverpool, Mario
Balotelli.
Endapo United itafanikiwa kuinasa saini ya Pogba,
huyo atakuwa mchezaji wa tano kununuliwa katika
utawala wa kocha mpya, José Mourinho baada ya
kufanikiwa kuwanasa mastaa Henrikh Mkhitaryan
kutoka Borussia Dortmund, Eric Bailly kutoka
Villarreal na Zlatan Ibrahimovic aliyenaswa bure
kutoka PSG.
Wakati Scholes akitoa maoni yake hayo kuhusu
Pogba, staa huyo wa zamani alitumia mwanya huo
kuwapongeza mahasimu wao, Manchester City,
ambao wametumia Pauni 21 milioni kumnasa staa
wa Borussia Dortmund, Ilkay Gundogan.
Scholes anaamini kwamba City wamelamba dume
kwa kumsajili staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani
mwenye asili ya Uturuki na atawasaidia sana kama
atafanikiwa kuepuka majeraha ya mara kwa mara
yanayomuandama.


Mwanaspoti



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top