Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia
Hanspoppe amesema hawatamuachia Laudit
Mavugo hata kama klabu ya Vital’O ya Burundi
inasema bado ina mkataba naye kwani wamefuata
taratibu zote kwenye usajili wake.
Rais wa Vital’O, Benjamin Bikorimana amesema
Mavugo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na
klabu hiyo, hivyo taarifa kuwa amemaliza mkataba
siyo za kweli.
“Simba wanapoteza muda na wanajisumbua kwani
Mavugo bado tuna mkataba naye, ITC (hati ya
uhamisho wake wa kimataifa) yake ipo kwetu, huyu
ni mchezaji wetu,” amesema Bikorimana.
Hanspoppe amesema kwa kiwango
alichokionyesha Mavugo kwenye tamasha la
‘Simba Day’, Jumatatu iliyopita hawatakubali
kumwachia na watapambana hadi haki yao
ipatikane
Hata hivyo, Hanspoppe amesema uongozi wa
Vital’O una matatizo na watahakikisha
wanakwenda hadi Fifa (Shirikisho la Soka la
Kimataifa) katika suala hilo.
“Sisi tunachojua Mavugo kamaliza mkataba, ila
baadhi ya viongozi wa Vital’O wana matatizo nasi
kwani mara ya kwanza tulipotaka kumchukua
Mavugo walisema bado ana mkataba wa miaka
miwili, tukamuacha hadi amalize ndipo tumchukue.
“Sasa hivi wanaibuka, wanasema ana mkataba wa
mwaka mmoja, sasa hatuwaelewi na huwa wana
matatizo tangu kipindi kile tunamchukua Tambwe
(Amissi), mambo yao yako hivyo hivyo.
“Wakigoma kutoa ITC tunakwenda Fifa kulalamikia
hili, nadhani huko ndipo haki itapatikana.
“Tunashangaa kwa nini wenzetu wanaficha
mikataba ya wachezaji, tukitaka kumchukua
mchezaji tukiwaambia tuonyeshe mkataba wake
umebaki muda gani hawasemi, hivyo wanaonyesha
ni watu wa shari,” amesema Hanspoppe.
Awali, Simba ilishindwa jaribio lake la kumsajili
mshambuliaji huyo na sasa imefanikiwa kunasa
saini yake, lakini tayari Vital’O inadai -usajili wake
ni batili.
Kinachofanywa na Viatal'O ni sawa sawa na
kilichofanywa na klabu ya Simba dhidi ya Yanga
juu ya usajili wa Hassan Kessy ambaye hadi leo
ameshindwa kuvaa uzi wa Yanga kwa kuwa Simba
imegoma kutoa kibali.
Simba wanadai Kessy bado ana mkataba wa
mwaka mmoja na klabu hiyo ingawa mwenyewe
amesema mkataba wake ulimalizika.
Posted: 👉👉 ⚽ Africa News Sports
Chapisha Maoni