MTALIANO Carlo Ancelotti amemwonya mwenzake Antonio Conte kuwa anapaswa kufanya usajili makini kwa sababu msimu ujao kikosi chake cha Chelsea kitakuwa na kazi kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo asiwe legelege.
Juzi Jumapili, Chelsea ilikamilisha usajili wake wa kwanza wa kutumia pesa wakati walipomnasa beki Antonio Rudiger kutoka AS Roma kwa ada ya Pauni 35 milioni na Mjerumani huyo amesaini mkataba wa miaka mitano Stamford Bridge.
Kiungo wa Monaco, Tiemoue Bakayoko naye anadaiwa kuwa yupo njiani kutua Chelsea huku mashabiki wa timu hiyo wakimjadili Rudiger kama kweli ni mchezaji atakayefaa kwenye mipango ya timu hiyo.
Ancelotti, ambaye aliwahi kuipa Chelsea mataji mawili ndani ya msimu mmoja miaka saba iliyopita, alisema hivi: “Conte atalazimika kufanya kitu tofauti. Alishinda ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini msimu mzima alionekana kuwatumia wachezaji walewale.
“Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya anahitaji kufanya usajili, tena anunue wengi na afanye ununuzi makini.”
Kwa msimu uliopita, Chelsea haikuwa na mzigo mkubwa wa michuano na walitumia nafasi hiyo kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu England, lakini msimu ujao watakuwa karibu kwenye michuano yote, hivyo wanapaswa kujipanga.
Chapisha Maoni