0
Wachezaji Michael Rushengonga na Dan Usengimana kutoka Rwanda wamewasili muda huu Dar es Salaam tayari kujiunga na Singida United.
Rusheshangonga alikuwa akichezea APR wakati Usengimana anatokea Polisi FC zinazoshiriki Ligi Kuu ya Rwanda.
Wachezaji hao wamepokelewa na Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga wakati walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Wakati wachezaji hao wakiwasili Kocha Mkuu wa Singida United, Hans Pluijm amesema anaona fahari kwa jinsi vijana wake wanavyobadilika kila siku na kwamba anasubiri kuanza kwa Ligi Kuu ili aanze kutembeza vipigo.
Singida ilitua jijini Mwanza Jumamosi iliyopita ikiwa kambini kujiandaa na Ligi Kuu ikijifua kwenye Uwanja wa Nyamagana na Butimba jijini hapa.
Pluijm alisema vijana wake wanampa raha kwa jinsi wanavyojifua na kubadilika kiwango kila kukicha.
Alisema kuwa kwa muda watakaokaa jijini hapa atahakikisha anawapa mazoezi tofauti tofauti ili kuwajenga kisaikolojia na fiziki ili ligi ikianza wasiwe na tatizo lolote kiufundi.
“Nafurahi kwa jinsi wanavyobadilika kila siku, wanafanya vizuri na sina wasiwasi, niseme kwamba nasubiri kuanza kwa ligi ili waitambue timu yangu na nitawaandaa vyema wachezaji haswa kiushindani,” alisema Pluijm.
Kocha huyo wa zamani wa Yanga, alisema anaamini timu hiyo itafanya vizuri na kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa kwani uwezo upo.
Aliongeza mchanganyiko wa wachezaji katika kikosi chake ndio moja ya kitu kitakachofanya timu kucheza kiushindani kwani kuna chipukizi na wazoefu hivyo kwa pamoja wataweza kufanya vizuri.
“Kwanza nina wachezaji mchanganyiko ni moja ya kitu kinachofanya timu kucheza kwa ushindani kila mmoja anakuwa na uwezo wake kwahiyo wakiungana wanafanya vizuri,” alisema Mdachi huyo.

Chapisha Maoni

 
Top