0

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga, amesema vijana wake wapo tayari kuibuka na ushindi jijini hapa.
Stars inavaana na Rwanda leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa katika mchezo wa kuwania kufuzu CHAN ambapo mchezo wa marudiano utacheza Kigali, Rwanda wikiendi ijayo.
Kuingia uwanjani kutazama mchezo huo utalipa kati ya Sh 5,000 na 10,000.
Mayanga ambaye tangu achukue mikoba ya kuifundisha timu hiyo ameiongoza kwenye mechi tisa na kufungwa mchezo mmoja pekee, alisema kuwa vijana wote wana ari na morali ya kusaka ushindi ili kusonga mbele na kwamba wamejipanga kushinda.
Alisema kuwa licha ya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kuwa na timu nzuri, amewaandaa vyema wachezaji kiushindani na anaamini hawatamwangusha.
“Kama ulivyoona hapa kwenye mazoezi kila mmoja anafanya vizuri, kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba tunakwenda kupambana na tuna imani kubwa ya kupata ushindi,” alisema.
Stars itaivaa Amavubi ikiwa na sura kadhaa mpya, lakini zenye vipaji na ikiwa ni wiki mbili tu tangu watoke Afrika Kusini walivyotwaa ushindi wa tatu katika michuano ya Kombe la Cosafa ambako ilikuwa timu mwalikwa.


Chapisha Maoni

 
Top