Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru)Mkoa wa Mwanza imesema inaendelea kufanya uchunguzi dhidi ya baadhi ya wagombea na wapiga kura katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) waliokamatwa jijini Mwanza wakibainika na makosa watapelekwa mahakamani.
Juzi Jumanne Takukuru iliwatia nguvuni jumla ya watu 10 wakiwamo wagombea wa nafasi za kamati tendaji TFF kwa madai ya kufanya kampeni kabla ya muda wake na kuwapo kwa viashiria vya utoaji rushwa, ambapo watuhumiwa waliachiwa kwa dhamana.
Mkurugenzi wa Takukuru mkoani Mwanza, Ernest Makale amesema uchunguzi unaendelea na kwamba wakipata ushahidi rasmi watawapeleka mahakamani.
"Bado tunazidi kufanya uchunguzi na ushahidi ukipatikana watuhumiwa watapandishwa mahakamani, tuliwaachia kwa dhamana," amesema Makale.
Ameongeza kuwa uchunguzi huo wanatarajia kuufanya haraka ili kabla ya uchaguzi mkuu wa TFF kufanyika, Agosti 12 wawe wameshakamilisha.
"Tunajua uchaguzi ni Agosti 12, sisi Takukuru tutahakikisha kabla ya muda huo tuwe tumeshakamilisha uchunguzi hawatapatikana na hatia, basi tutazungumza nao," amesema Makale.
Viongozi na wapiga kura waliokamatwa ni Shaffih Dauda, Ephrahim Majinge, Elias Mwanjala, Leonard Malongo, Osuli Osuli, Richard Kiyenze, Patrick Chila, Razack Juma na Akmas Kasongo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni